*WAZIRI MKUU KUANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI ARUSHA FEBRUARI 22–24, 2026
*Kukagua miradi ya kimkakati na kuzungumza na wananchi wa Arumeru, Longido na Arusha
*RC Makalla awaalika wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya hadhara
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Arusha kuanzia Februari 22 hadi 24, 2026, akilenga kukagua na kuzindua miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 194.2 pamoja na kuzungumza na wananchi wa wilaya za Arumeru, Longido na Jiji la Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kijamii na kiuchumi, kusikiliza kero za wananchi na kutoa maelekezo ya papo kwa papo ili kuongeza kasi ya maendeleo mkoani humo.
Ratiba ya Siku ya Kwanza – Arumeru
Kwa mujibu wa Makalla, siku ya kwanza ya ziara, Jumapili Februari 22, Waziri Mkuu ataanza kwa kuweka jiwe la msingi la bweni la kisasa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Sayansi cha Nelson Mandela, mradi unaolenga kuongeza uwezo wa udahili na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Baadaye atakagua upanuzi wa miundombinu ya Hospitali ya Oltrumet kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Ngaramtoni, akitoa mrejesho wa utekelezaji wa miradi na kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya, maji na miundombinu.
Siku ya Pili – Longido na Namanga
Tarehe 23 Februari, Dkt. Nchemba atatembelea Wilaya ya Longido ambako atapokea taarifa ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Sinya, mradi unaotarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, atazindua upanuzi wa Shule ya Sekondari Sinya iliyoboreshwa na kuwa na kidato cha tano na sita, hatua inayolenga kupanua fursa za elimu ya juu kwa vijana wa wilaya hiyo. Vilevile, atatembelea One Stop Border Post Namanga kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Msingi Namanga.
Siku ya Tatu – Jiji la Arusha
Katika siku ya mwisho ya ziara yake, Waziri Mkuu atakagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Jiji la Arusha katika eneo la Bondeni City, mradi unaotarajiwa kuboresha usafiri wa abiria na biashara. Pia ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Soko la Kilombero na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika eneo hilo.
Wito kwa Wananchi
RC Makalla amewaalika wananchi, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ya mikutano ya hadhara ili kusikiliza hotuba ya Waziri Mkuu na kuwasilisha maoni yao kuhusu vipaumbele vya maendeleo ya mkoa.
Amesema ziara hiyo ni fursa muhimu ya kujenga uwajibikaji, kuongeza uwazi katika utekelezaji wa miradi ya umma na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Arusha.
Ends...



0 Comments