SERIKALI YASHUSHA GHARAMA ZA KUSAJILI ONLINE TV HADI 50,000

By Arushadigital

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepunguza kwa kiwango kikubwa ada za usajili wa vyombo vya habari mtandaoni, hatua inayolenga kuwezesha wamiliki wa blogu, Online TV na majukwaa ya kidijitali kufanya kazi zao kwa urahisi na gharama nafuu.


Kupitia maboresho hayo, ada ya leseni kwa vyombo vya habari mtandaoni imepunguzwa kutoka shilingi 500,000 hadi shilingi 50,000, huku ada ya maombi ya leseni ikishushwa kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 10,000 pekee. Hatua hiyo imeelezwa kuwa mkombozi kwa wanahabari na wajasiriamali wa sekta ya habari nchini.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na TCRA katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya sekta ya habari ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya jamii.


Mwinjuma pia ameiagiza TCRA kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha madai ya mishahara na stahiki za wafanyakazi wa vyombo vya habari yanashughulikiwa kwa haraka, akisisitiza kuwa ndani ya wiki moja anatarajia kupokea taarifa ya hatua zilizochukuliwa.


Hata hivyo amesema Serikali itaendelea kulinda haki ya wananchi kupata taarifa, huku akihimiza vyombo vya habari kuzingatia maadili ya taaluma, kuongeza ubora wa maudhui na kulinda haki miliki.

Post a Comment

0 Comments