MWANAFUNZI SHULE YA IMANI AVUNJWA MKONO KWA KIPIGO CHA WALIMU SHULENI ARUSHA,ATIMULIWA SHULE NA ADA YAREJESHWA ,WIZARA YA ELIMU , WAZIRI GWAJIMA WATAKIWA KUINGILIA KATI, NI ZAIDI YA MWEZI MTOTO YUPO NYUMBANI

 MWANAFUNZI AVUNJWA MKONO  KWA KIPIGO CHA WALIMU SHULENI ARUSHA

Walimu wawili wakamatwa, mmoja anatafutwa na polisi baada ya kukimbia

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


MWANAFUNZI wa darasa la tano, Blessing Ramale, wa Shule ya Msingi Imani (English Medium) iliyopo Sombetini, jijini Arusha, amevunjwa mkono wa kushoto kwa kipigo cha walimu watatu na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kwa madai ya kutofanya kazi ya nyumbani(HomeWork).


Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa kuhusu usalama wa wanafunzi na utekelezaji wa miongozo ya adhabu mashuleni, huku familia ya mtoto ikitaka hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika.


Akisimulia tukio hilo kwa maumivu nyumbani kwa wazazi wake, Blessing alisema alipigwa kwa fimbo darasani na walimu wawili na baadaye kutolewa nje na mwalimu aliyemtaja kwa jina moja la Samsom, ambapo kipigo kiliongezeka hadi zaidi ya fimbo 15 na kulazimika kukimbilia ofisi ya walimu ,lakini aliendelea kushambuliwa na kupatwa na maumivu makali ya Mkono,wakimtuhumu kitofanya 'homework' na masomo darasani


“Nilikuwa naumia sana… niliomba waache lakini walizidi kunipiga. Mkono wangu wa kushoto ulikuwa unauma sana,” alisema mwanafunzi huyo, akieleza kuwa hakuweza kuendelea na masomo siku hiyo kutokana na maumivu makali.


Kwa mujibu wa familia, mwanafunzi huyo alipelekwa katika Hospitali ya Mount Meru ambako vipimo vilibaini kuvunjika kwa mfupa wa mkono (fracture) pamoja na majeraha ya kipigo sehemu mbalimbali za mwili.


Akizungumza kwa uchungu, mama mzazi wa mtoto, Jackline John, alisema tukio hilo limebadili kabisa hali ya maisha ya mwanawe.


“Mtoto alikuwa anajihudumia mwenyewe, sasa analishwa na kuogeshwa. Maumivu ni makali na madaktari wamependekeza uchunguzi wa kina zaidi,” alisema.


Aliongeza kuwa familia ilifungua jalada polisi na kwamba maafisa elimu pamoja na wakaguzi walifika shuleni kuanza uchunguzi.

“Tunataka haki ya mtoto ilindwe na wahusika wawajibishwe ila hatutaacha kuiahukuru wizara ya Elimu pamoja na wizara ya maendeleo ya jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalumu kwa ushirikiano wa hatua za awali katika tukio hili "  alisisitiza.


Kwa mujibu wa taarifa za polisi, walimu wawili walikamatwa shuleni hapo na baadaye kudhaminiwa, huku mwalimu mmoja anayedaiwa kumpiga mwanafunzi fimbo nyingi zaidi na kusababisha kuvunjika mkono akitoroka na kwa sasa anatafutwa na vyombo vya dola.


Babu wa mtoto huyo, John Nyegu, alisema Blessing anaendelea na matibabu nyumbani chini ya uangalizi wa familia huku akihitaji msaada wa karibu katika shughuli za kila siku.


Kwa upande wake, mmiliki wa shule hiyo, Martha Kasago, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukamatwa kwa walimu wawili, akisema hakutoa maelekezo ya adhabu kali kwa mwanafunzi. Alisema ada ya mwanafunzi ilirejeshwa na mzazi alichagua kumwondoa shuleni hapo.

Hata hivyo alisisitiza kuwa mtoto alijiunga na shule akiwa na matatizo ya mkono na siku ya tukio aliguswa kidogo tu na kupata madhara.

“Kwa kuwa suala lipo kwenye vyombo vya sheria, tuviachie vifanye kazi yake ili haki ipatikane,na huyu mwalimu Samson sijamficha aliamua kukimbia mwenyewe baada ya kusikia tukio hilo limefika po Li si,” alisema.


Hata hivyo, familia imepinga kauli ya uongozi wa shule ikisisitiza kuwa tukio hilo ni la ukatili usiovumilika katika mazingira ya elimu.


Hadi tunakwenda mitamboni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha pamoja na mamlaka za elimu walikuwa wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.


 Familia imetoa wito kwa serikali na wadau wa elimu kuimarisha ulinzi wa watoto na kuweka mipaka madhubuti ya adhabu mashuleni.


Tukio hilo linaongeza msukumo wa mjadala wa kitaifa kuhusu wajibu wa taasisi za elimu kulinda ustawi na haki za wanafunzi.

Kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto, utambulisho na sura yake vimehifadhiwa.”

Ends..

Post a Comment

0 Comments