MAKALA MAALUM | KIFO CHA BANJOO CHAAMSHA TAHARUKI ARUSHA: LHRC YAHOJI USALAMA SEKTA YA MADINI, POLISI WASISITIZA UCHUNGUZI UNAENDELEA

 MAKALA MAALUM | KIFO CHA BANJOO CHAAMSHA TAHARUKI: LHRC YAHOJI, POLISI WASISITIZA UCHUNGUZI UNAENDELEA

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA



KIFO cha mfanyabiashara na mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Abdilah Mussa “Banjoo”, kimeendelea kuzua maswali mazito kuhusu usalama wa wafanyabiashara wa madini na uwajibikaji wa taasisi za dola.


 Marehemu alitoweka katikati ya Februari 2026 na baadaye mwili wake kupatikana katika eneo la Bereko, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma—tukio lililotikisa jamii na wadau wa sekta ya vito.


Kwa mujibu wa Legal and Human Rights Centre (LHRC), Banjoo alichukuliwa na watu wasiojulikana Februari 12, 2026 alipokuwa akifanya mazoezi nje ya jengo la Ngorongoro, jijini Arusha. 


Baada ya kupotea kwa takribani wiki moja, mwili wake ulipatikana Februari 19, 2026, hali iliyozidisha hofu na sintofahamu miongoni mwa wananchi.


Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, limethibitisha kupokea taarifa za kupotea kwa Banjoo Februari 13, 2026, ikielezwa kuwa alionekana mara ya mwisho Februari 12, 2026.


Kamanda Masejo amesema kuwa wakati uchunguzi ukiendelea, Februari 19, 2026 Polisi walipokea taarifa kwamba mtu huyo amefariki dunia huko mkoani Dodoma.


 Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kukusanya taarifa na vielelezo vinavyohusiana na tukio hilo, huku akitoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kujitokeza mara moja.


“Tunapokea na kufanyia kazi kwa haraka taarifa zote zinazoweza kusaidia kufanikisha uchunguzi huu,” amesisitiza Kamanda Masejo.


Kupitia taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Anna Henga, LHRC imelaani mauaji hayo na kuhoji ucheleweshaji wa taarifa rasmi kwa umma. 


Taasisi hiyo imesisitiza kuwa tukio hilo linagusa haki ya kuishi kama inavyolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na kuonya kuwa ukosefu wa uwazi unaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa vyombo vya dola.


Taarifa ya kina kuhusu mwenendo wa uchunguzi,Kusakwa na kufikishwa mahakamani kwa wahusika,Kuundwa kwa Tume Huru ya Kijaji kuchunguza tukio hili na matukio yenye mfanano wake.


Kisa cha Banjoo kimefufua kumbukumbu za matukio ya nyuma yanayohusishwa na wafanyabiashara wa madini katika ukanda wa kaskazini, yakiwemo mauaji ya mfanyabiashara mashuhuri wa vito Erasto Msuya mwaka 2013. 


Wachambuzi wanaeleza kuwa ushindani mkali, miamala mikubwa ya fedha taslimu, na mikataba isiyo rasmi vinaweza kuongeza hatari za migogoro na uhalifu unaolenga watu binafsi.


Kwa Arusha—kitovu cha biashara ya Tanzanite—usalama wa wadau ni sehemu ya miundombinu ya uchumi. Mfululizo wa matukio ya kutatanisha unaweza kuathiri imani ya wawekezaji na taswira ya soko la vito kimataifa.


Wakati Polisi wakisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na kuhimiza ushirikiano wa umma, wadau wa haki za binadamu na wafanyabiashara wa madini wanasisitiza uwazi, kasi, na uwajibikaji.


Kesi ya Banjoo imeibua maswali mazito juu ya ufanisi wa mifumo ya ulinzi na mustakabali wa biashara ya madini nchini.Banjoo amezikwa leo nyumbani kwake Sanawari na halaiki ya watu huku maziko yakitawaliwa na vilio na Simanzi na watu kuzimia


Ends..

Post a Comment

0 Comments