MIUNDOMBINU YA UMMA ARUSHA YATEKETEA: JIJI LAOMBA BILIONI 1.866 KWA UKARABATI WA HARAKA
Ofisi za kata na mitaa zaharibiwa katika vurugu za uchaguzi; huduma kwa wananchi zatetereka — Baraza la Madiwani latakiwa kuidhinisha fedha 2026/27
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
HALMASHAURI ya Jiji la Arusha imetangaza hitaji la dharura la shilingi bilioni 1.866 kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya umma iliyoharibiwa katika vurugu za uchaguzi na baada ya uchaguzi, zilizosababisha kuchomwa kwa majengo ya serikali na kuathiri moja kwa moja utoaji wa huduma katika ngazi za kata na mitaa.
Akizungumza leo februali 13,2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani, Kaimu Mkurugenzi wa jiji, Dkt. Maduhu Nindwa, alisema tathmini ya awali imebaini uharibifu mkubwa wa ofisi za watendaji wa kata na mitaa, nyaraka za kiutawala, pamoja na vifaa vya ofisi, hali iliyosababisha kusuasua kwa huduma muhimu kwa wakazi wa Arusha.
Hoja hiyo iliibuliwa kupitia swali la papo kwa papo lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Baraa, Jacob Meja, aliyetaka kujua ratiba ya kurejesha miundombinu hiyo na hatua za haraka za kurejesha utendaji wa ofisi zilizoathirika.
“Wakati matukio haya yakitokea, bajeti ya halmashauri ilikuwa tayari imepitishwa. Hivyo, tunaliomba Baraza la Madiwani kuidhinisha ombi la fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ili ukarabati ufanyike kwa wakati na huduma zirejee katika hali ya kawaida,” alisisitiza Dkt. Nindwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa jiji, uharibifu huo umeathiri shughuli za kiutawala na utoaji wa huduma za msingi ikiwemo usajili wa wakazi, uratibu wa miradi ya maendeleo ya mitaa, pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani. Baadhi ya ofisi zimekuwa zikitoa huduma kwa muda kwa kutumia maeneo mbadala yasiyo na miundombinu stahiki.
"Baada ya uharibifu wa vurugu za uchaguzi oktoba 29,2026 Tathimini ya kwanza iliyofanyika katika maeneo yote ya mitaa na kata kiasi cha sh bilioni 1.866 zinahitajika "Alisema dkt Maduhu.
Wadau wa maendeleo na viongozi wa kijamii jijini humo wameitaka halmashauri, sambamba na ukarabati, kuweka mikakati madhubuti ya ulinzi wa miundombinu ya umma na kuimarisha mifumo ya tahadhari ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika siku zijazo.
Baraza la Madiwani linatarajiwa kujadili na kuidhinisha ombi hilo katika mchakato wa bajeti ijayo, hatua itakayofungua njia ya ukarabati wa majengo, ununuzi wa vifaa na kurejesha utendaji kamili wa ofisi za serikali za mitaa.
Kwa sasa, macho ya wakazi wa jiji la Arusha yanaelekezwa kwa uamuzi wa baraza hilo, wakitarajia hatua za haraka zitakazorejesha huduma bora na kuimarisha utawala wa karibu kwa wananchi.
— MWISHO —



0 Comments