SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA AFYA NA MIUNDOMBINU ARUSHA
Na Joseph Ngilisho – Arusha
MBUNGE wa Arumeru Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amesema serikali inaendelea kuweka mkazo katika utoaji wa huduma bora za afya na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Akizungumza leo februari 20,2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC), Dkt. Lukumay alieleza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za afya kwa urahisi bila vikwazo, sambamba na kuboresha miundombinu inayochochea ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi.
Alisema maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona ifikapo mwaka 2030 Watanzania wanaishi kwa furaha na afya njema kupitia utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya kwa wote. Alibainisha kuwa kupitia mpango huo, makundi maalum ikiwemo watoto chini ya miaka mitano, wazee, wanawake wajawazito pamoja na wananchi wanaoishi katika kaya zenye kipato cha chini watanufaika na huduma za afya bila malipo.
Kwa mujibu wake, serikali pia inaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa ili kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa huduma bora na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma nchini.
Akizungumzia miundombinu, mbunge huyo alisema serikali imeanza kuona matokeo ya uwekezaji katika barabara, lakini bado kuna haja ya kuongeza kasi ya uboreshaji wa barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo mbalimbali ya Arusha, ikiwemo barabara za Sanawari–Bangata na Mbenda–Losinyenye pamoja na ujenzi wa madaraja muhimu.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuongezwa kwa bajeti ya TARURA ili kuwezesha ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja, akieleza kuwa ongezeko la rasilimali litaimarisha usafiri, kurahisisha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Lukumay aliomba ushirikiano wa madiwani katika kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika kata mbalimbali.
Aidha mbunge alikerwa na kitendo cha baadhi ya wakuu wa idara ya halmashuri hiyo kutotoa taarifa pindi anapohitaji kwa lengo la kuwajulisha wananchi kuhusu maendeleo ya jimbo lao
Alisisitiza umuhimu wa mawasiliano ya karibu kati ya viongozi ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akionesha masikitiko yake kwa baadhi ya madiwani kutopokea simu anapohitaji taarifa kuhusu hali ya maendeleo na changamoto zilizopo.
Alimalizia kwa kuwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali katika juhudi za kuimarisha sekta ya afya na miundombinu, akisisitiza kuwa hatua hizo ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya taifa.
Ends












0 Comments