KASI YA MBUNGE ARUMERU MAGHARIBI INATISHA ATEMBELEA MRADI WA MAJI WA MILIONI 385 KIRANYI ,ATOA MAELEKEZO MAZITO AUWSA

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU

 


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameielekeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (AUWSA) kuhakikisha inakamilisha kwa wakati mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Kiranyi, wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 385.


Dkt. Lukumay alitoa agizo hilo leo dec 4,2025 wakati alipotembelea eneo la mradi na kukagua hatua zilizofikiwa, akibainisha kuwa juhudi hizo ni sehemu ya kasi yake ya kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi wa jimbo hilo, hususan katika kuhakikisha kila kaya inapata huduma ya uhakika ya maji safi.

> “Wananchi wanahitaji maji safi ya kunywa. Huu ni mradi mkubwa na wenye manufaa makubwa, hivyo nawahimiza mkamilishe kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika mapema iwezekanavyo,” alisema Dkt. Lukumay.


Mbunge huyo pia aliutaka uongozi wa Kata ya Kiranyi, akiwemo Diwani Elius Lukumay, kuimarisha elimu ya ulinzi wa miundombinu ya maji kufuatia taarifa kuwa baadhi ya wakazi wamekuwa wakiharibu mabomba ya usambazaji.

> “Hatuwezi kukubali mradi wa thamani kubwa kama huu upate uharibifu. Viongozi wa kata msimamie, elimu itolewe, na wananchi wajue hii ni mali yao — lazima ilindwe,” 

 

Awali, Meneja wa AUWSA Kanda ya Kati, Restituta Charles, alieleza kuwa mradi huo wa ujenzi wa matenki ya kuhifadhi na kusambaza maji umefikia hatua ya kuridhisha, ambapo hadi sasa umefika asilimia 88 ya utekelezaji.

Alisema kazi zilizobaki ni za mwisho mwisho, na kwamba mamlaka yake imejipanga kuhakikisha mradi unakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu, ili wananchi waanze kupata maji safi bila kuchelewa.

> “Mradi huu ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Kiranyi. Kukamilika kwake kutanufaisha kaya zaidi ya 3,650. Tunapata maji ya kutosha kutoka visima na chanzo cha chemchemu ya Kirani, na maji yote yatapitia kwenye tanki hili lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 50 kwa ajili ya kutibiwa kabla ya kusambazwa kwa wananchi,” alisema Restituta.

Alimshukuru Mbunge Dkt. Lukumay kwa kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi, akisema msukumo wake umesaidia kuongeza kasi ya kukamilisha shughuli za ujenzi.

> “Tunakushukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji na msukumo wenu. Mmeongeza ari kwa timu yetu kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa viwango na kwa muda uliopangwa,” alisisitiza.


Diwani wa Kata ya Kiranyi, Elias Lukumay, alisema wakazi wa kata hiyo wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu, hivyo mradi huo ni suluhisho muhimu.

Alitoa rai kwa wananchi kushirikiana kulinda miundombinu ili mradi huo uwe endelevu.

> “Tunaomba wananchi tushirikiane kulinda miundombinu hii. Mradi huu unamaliza changamoto ya maji Kiranyi,” alisema.








Ends

Post a Comment

0 Comments