POLISI YAWASAKA VIGOGO NANE WA CHADEMA AKIWEMO GWAJIMA,GOLUGWA AKAMATWA NYUMBANI KWAKE

By Arushadigital


JESHI la Polisi limesema linawatafuta Josephati Gwajima, Godbless Lema, na wengine nane wakiwemo Brenda Rupia, John Mnyika, Machumu Kadutu, Deogratius Mahinyila, Boniface Jacob, Hilda Newton, Award Kalonga na Amaan Golugwa.

Hata hivyo Taarifa zilizotufikia punde zinadai kuwa tayari jeshi hilo limemkamata na kumshikilia makamu mwenyekiti wa Chadema ,Amani Golugwa aliyekamatiwa nyumbani kwake jijjni Dar es salaam

Polisi inasema hatua hiyo imekuja kufuatia matukio ya vurugu, uporaji wa mali na uvunjifu wa amani yaliyotokea tarehe Oktoba 29, mwaka huu katika majiji ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya.


Pia katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Songwe, Ruvuma, Mara, Dodoma, Kilimanjaro na Iringa na kusababisha madhara kwa binadanu, kuharibu mali nyingi za umma na za watu binafsi na kulileta athari kubwa.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, mbali na athari kwa uhai na maisha ya watu, waliofanya uhalifu huo waliharibu na kuchoma moto mali za umma kama vile Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).


Maeneo mengine ni Mahakama, ATM za baadhi ya Benki, Vituo vya Polisi, Vituo vya Mabasi ya Mwendo kasi kutoka Kimara mwisho hadi Magomeni na kutoka Magomeni hadi Moroco, Ofisi za Serikali za Mitaa, kuchoma moto barabara za lami na za zege kwa kutumia matari na majengo kadhaa ya Chama cha Mapinduzi. Pia walichoma moto na kuharibu magari ya umma.


“Mali za watu binafsi zilizoharibiwa na kuchomwa moto, ni pamoja na Vituo vya Mafuta, maduka mbalimbali, magari makubwa na madogo, pia walifanya uporaji wa mali na pesa za watu kutoka maeneo mbalimbali ya biashara.

“Baadhi ya waliopanga na kutekekeza uhalifu huo wamekamatwa na kuanza kufikishwa mahakamani, pia Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta wale wote waliopanga, kuratibu na kutekeleza uovu huo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.



Imeongeza kwamba wakati hatua hizo zikiendelea, jamii inaombwa kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kutoa taarifa za watu wote waliohusika ili hatua sahihi za kisheria zichukuliwe dhidi yao.


Aidha, Jeshi la Polisi limewataka watu wote waliotajwa hapo juu kujisalimisha katika vituo vya polisi mara moja watakapoona taarifa hiyo popote pale walipo.


Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi linawafahamisha kuwa, hatua za kisheria kwa wahalifu ambao wamekwishakamatwa zinaendelea kote nchini na kwamba jana baadhi wamefikishwa mahakamani.


“Jeshi la Polisi linaonya kuwa, mtu au kikundi cha watu wanaopanga kufanya uhalifu wa namna yoyote ile halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao. Pia, Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi katika kulinda raia na mali zao,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.



Hata hivyo, imeeleza umma kuwa, waendelee na shughuli zao bila hofu yeyote na watoe taarifa mara moja pale wanapoona dalili yoyote ya uhalifu ama uvunjifu wa amani mahali popote pale ili hatua kwa mujibu wa sheria ziweze kuchukuliwa.


“Taarifa zitaendelea kutolewa kadri hatua za kisheria zinavyoendelea kuchukuliwa dhidi ya waliotenda uhalifu huo na wanaoendelea kupanga uhalifu wa aina yeyote ile,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Post a Comment

0 Comments