BAADA YA KUTEULIWA WAZIRI MKUU ,MWIGULU APANGA KUFYEKA UMASKINI NCHINI

 By Arushadigtal -DODOMA

 Dkt. Mwigulu Nchemba: “Umaskini wa Watanzania sijauona kwenye vitabu, nimeuishi”


WAZIRI MKUU mteule, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameapa kushughulikia kwa nguvu zote watumishi wazembe, wala rushwa na wenye kauli mbaya kwa wananchi, akisisitiza kuwa wakati umefika wa Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anahudumiwa kwa heshima na uadilifu.

Akizungumza leo, Novemba 13, 2025, mara baada ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumthibitisha rasmi kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Nchemba alisema licha ya Tanzania kuwa nchi tajiri kwa rasilimali, bado takribani asilimia 8 ya Watanzania wanaishi katika umaskini wa kupindukia, huku asilimia 26 wakiishi kwa mlo mmoja kwa siku.

> “Mimi umaskini wa Watanzania sijausoma kwenye vitabu, nimeuishi. Mheshimiwa Spika, katika maisha yangu haya na umri wangu huu, takribani miaka 32, nimeishi maisha ya umaskini. Nilikuwa najifunika nguo aliyokuwa anajifunga shemeji yangu,” alisema Dkt. Nchemba kwa hisia.

Mwigulu akikaribishwa ofisini 

Ameeleza kuwa uzoefu huo wa maisha ya kijijini ndio unaompa msukumo wa dhati wa kuhakikisha Serikali inaboresha maisha ya wananchi wote bila ubaguzi.

> “Watumishi wa umma na Watanzania wote lazima twende kwa gia ya kupandia mlima, twende na gia ya kupita baharini yenye mawimbi na anga lenye mawingu, chombo kifike salama na watu wake wakiwa salama,” alisisitiza.


Ameonya kuwa katika Serikali yake, hakutakuwa na nafasi kwa uvivu, uzembe, wala lugha chafu kwa wananchi, na kwamba atahakikisha utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais unafanyika kwa kasi na nidhamu kubwa.

> “Wale watumishi wazembe, wavivu, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania — tuwe tayari, nitakuja na fyekeo na rato. Maono ya Mheshimiwa Rais lazima yatekelezwe,” alionya Dkt. Nchemba.


Kauli hiyo imeibua matumaini mapya miongoni mwa wananchi wengi wanaotamani kuona mabadiliko ya kweli katika utendaji wa Serikali, hasa katika utoaji wa huduma kwa wananchi wa kawaida vijijini na mijini.




#Arushadigital#

Post a Comment

0 Comments