WATAALAMU WA AFYA NA WACHUNGAJI NCHINI,WAHITIMU MAFUNZO YA TIBA SHUFAA NA HUDUMA YA FARAJA KUPITIA HOSPITAL I YA ALMC

 Wataalam wa Afya 32 Wahitimu Mafunzo ya Tiba Shufaa na Huduma ya Faraja ALMC

Serikali yatenga bajeti maalum kuimarisha huduma za tiba shufaa nchini


Na Joseph Ngilisho — Arusha

WATAALAMI  32 wa afya kutoka mikoa mbalimbali nchini wamehitimu mafunzo maalum ya Tiba Shufaa na Huduma ya Faraja, yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuwapatia wagonjwa unafuu na matumaini mapya ya kuendelea kuishi. 


Mafunzo hayo yametolewa na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kupitia Kitengo cha Programu ya Tiba Shufaa na Huduma ya Faraja.

Hafla ya kufunga mafunzo hayo ya wiki mbili ilifanyika leo alhamis ,oktoba 16,2025 Katika kituo hicho cha Selian Tiba Shufaa kilichopo Ilboru  Arusha na kuongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ALMC, Dkt. Godwill Kivuyo, ambaye pia aliwatunuku vyeti wahitimu hao wakiwemo madaktari, wauguzi na wachungaji kutoka taasisi mbalimbali za afya nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kivuyo alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaongezea washiriki ujuzi wa kutoa huduma za tiba na kiroho kwa wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyotibika, ili kuwapa faraja na matumaini mapya.

“Tunawasisitiza wahudumu wa afya, wakiwemo madaktari bingwa waliopatiwa mafunzo haya, kuyatumia kwa vitendo kuwapatia wagonjwa huduma ya unafuu na kuwafanya waongeze siku za kuishi. Pia tunawahimiza wakafundishe wengine katika vituo vyao ili kuongeza wigo wa huduma hii nchini,” alisema Dkt. Kivuyo.



Aidha, alibainisha kuwa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeona umuhimu wa huduma za tiba shufaa na faraja, na tayari imeweka bajeti maalum kuhakikisha huduma hizo zinaendelezwa kwa upana zaidi nchini.

“ALMC imekuwa hospitali ya kwanza kuanzisha huduma hii hapa nchini, na tunafarijika kuona serikali ikiunga mkono juhudi hizi kwa vitendo, ikiwemo kutenga bajeti kupitia wizara husika,” aliongeza Dkt. Kivuyo.


Alisema mafunzo hayo yamewezeshwa na wabobezi wa afya kutoka Marekani, waliotoa elimu ya kitaalamu kuhusu mbinu za kisasa za utoaji huduma ya faraja kwa wagonjwa wanaopitia changamoto za kiafya, kiakili na kisaikolojia.


Kwa upande wake, Mratibu wa Kitengo cha Selian Tiba Shufaa na Huduma ya Faraja, Tumaini Kweka, alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu endelevu inayotolewa kila mwaka kwa wataalamu wa afya kutoka hospitali mbalimbali zilizo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

“Tangu tulipoanza kutoa mafunzo haya mwaka 2011, zaidi ya wataalamu 240 wa sekta ya afya kutoka mikoa mbalimbali nchini wamepata mafunzo haya. Tunahusika pia kutembelea wagonjwa hospitalini na majumbani wanaougua magonjwa yasiyotibika, tukiwapatia huduma za kimwili, kiroho na kijamii,” alisema Kweka.


Kweka aliongeza kuwa huduma hizo zimekuwa na matokeo chanya kwa wagonjwa waliokuwa wamekata tamaa, kwani wengi wao wameanza kuonyesha matumaini mapya na kuongezeka kwa siku za kuishi.

“Tunawatembelea pia majumbani na kuwapatia mahitaji kama chakula na nguo, hasa wazee na watoto waliobaki bila wazazi baada ya kufariki kwa magonjwa mbalimbali. Huduma hii imeleta matokeo makubwa ya kibinadamu,” alifafanua.


Kwa upande wake, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Dkt. Anna Mushi kutoka Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro (Machame), alisema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa kwa undani umuhimu wa kutoa huduma zenye kugusa utu wa mgonjwa.

“Tulikuwa tunajikita zaidi kwenye tiba ya mwili pekee, lakini sasa tumejifunza kwamba wagonjwa wa magonjwa yasiyotibika wanahitaji pia huduma ya kiroho na faraja. Hii elimu tutaipeleka kwenye hospitali zetu na kuwafundisha wenzetu ili huduma hii iwe endelevu,” alisema Dkt. Mushi.


Mafunzo hayo yameelezwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya jumuishi nchini, zinazogusa si tu mwili wa mgonjwa bali pia nafsi na roho yake — kwa lengo la kumrudishia matumaini, utu na hadhi ya kuishi kwa amani na faraja.









 










Ends.


Post a Comment

0 Comments