SEKEYANI AZINDUA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA TERAT, ATOA AHADI KUBWA – WANANCHI WAMPONGEZA
Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
MGOMBEA udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Terat, Julias Ole Sekeyani, leo Oktoba 4,2025 amezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Bondeni Kati, uliovutia mamia ya wananchi na wafuasi wa chama hicho.
Uzinduzi huo umefanyika zaidi ya mwezi mmoja tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu Agosti 28, 2025, ambapo Sekeyani aliwahakikishia wananchi kuwa CCM haikukosea kumteua kwani ana uzoefu na uwezo wa kusukuma maendeleo katika kata hiyo.
Akihutubia umati wa watu, Sekeyani aliahidi miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa shule tatu za msingi, maboresho ya barabara, na upatikanaji wa maji safi na salama.
> “Nitarudisha heshima ya Terat. Kwa ushirikiano wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wetu Ndugu Paulo Makonda, katika miaka mitano ijayo tutaona mageuzi makubwa ya kimaendeleo. Terat haitabaki pale ilipo,” alisema Sekeyani kwa kujiamini.
Sekeyani, ambaye aliwahi kuwa diwani wa kata hiyo, alisisitiza kuwa anarudi na nguvu mpya kuhakikisha changamoto za wananchi zinabaki historia.
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM, Saipulani Ramsey, alimkabidhi Sekeyani Ilani ya Uchaguzi akimtaka kuitumia kama mwongozo wa kuwaletea wananchi maendeleo.
> “Sekeyani ni mchapakazi na ndiye kiongozi anayehitajika. Na nakuagiza, hakikisha barabara ya Mkonoo hadi Bypass inajengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa adha ya usafiri wakati wa mvua,” alisema Ramsey.
Ramsey pia hakusita kuwashukia wapinzani akidai hawana sera madhubuti zaidi ya kutoa ahadi zisizotekelezeka.
> “Wapinzani ni maneno matupu. Wao kila siku ni kulaumu na kulalamika, lakini CCM inakuja na miradi. Wananchi wa Terat msidanganyike, maendeleo hayaji kwa maneno, bali kwa vitendo na utekelezaji wa Ilani ya CCM,” alisema huku akishangiliwa.
Mwenyekiti wa UWT Kata ya Terat, Mary Kisaka, aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura kwa ajili ya kumchagua diwani wa CCM, Mbunge na Rais ili kuendeleza ushindi wa chama hicho.
Wananchi pia walionyesha imani kubwa kwa Sekeyani. Rehema John, mkazi wa eneo hilo alisema:
> “Sekeyani si mtu wa maneno matupu. Wakati akiwa diwani alituletea maji safi, tunaamini safari hii atatufungulia miradi mikubwa zaidi.”
0 Comments