MHASIBU AHUKUMIWA KWA KUGHUSHI SAHIHI, AIBA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 5 ZA ZAHANATI
Na Joseph Ngilisho- Arushadigital
BABATI, MANYARA – Mahakama ya Wilaya ya Babati imemtia hatiani Mohamed Twalib Baya, aliyekuwa mhasibu, baada ya kupatikana na hatia ya kughushi sahihi za watia saini katika akaunti ya Zahanati ya Gidas na kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Katika shauri la Jinai Na. 2979/2026, mahakama hiyo ilibainisha kuwa mshtakiwa alighushi sahihi za watia saini wa akaunti ya zahanati hiyo na kisha kuchukua fedha jumla ya Shilingi 5,426,000, ambazo alizifanyia ubadhirifu.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Babati, Mheshimiwa Victor Kimario, alisema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa baada ya kufikia makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Kutokana na kukiri kosa hilo, mahakama ilimhukumu mshtakiwa kifungo cha miezi mitatu jela pamoja na kurejesha fedha zote alizozifanyia ubadhirifu kwa muathirika.
Ilielezwa kuwa hadi hukumu inasomwa mahakamani, mshtakiwa tayari alikuwa amerejesha kiasi chote cha Shilingi 5,426,000 katika akaunti ya Zahanati ya Gidas iliyopo katika Benki ya NMB, tawi la Muhanga.
Shauri hilo liliendeshwa na timu ya waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, wakiongozwa na mawakili Neema Gembe, Davis Masambu na Catherine Ngessy.
Mahakama ilisisitiza kuwa vitendo vya kughushi nyaraka na ubadhirifu wa fedha za taasisi za umma havitavumiliwa, huku ikitoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia uadilifu na kuwajibika katika usimamizi wa rasilimali za umma.

0 Comments