MKOA WA ARUSHA WAOMBA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 503.9 KWA MWAKA WA FEDHA 2026/

 MKOA WA ARUSHA WAOMBA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 503.9 KWA MWAKA WA FEDHA 2026/2027

*Makalla asisitiza ushirikiano kusimamia miradi ya maendeleo na miundombinu

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKOA wa Arusha umeomba kuidhinishiwa mapendekezo ya bajeti ya jumla ya Shilingi bilioni 503.995 kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na uendeshaji wa Serikali katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC), ambapo wajumbe waliombwa kuyapitia na kuyaidhinisha ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Mkoa huo.

Akiwasilisha taarifa ya mapendekezo hayo, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Mipango,  Apolinary Seiya, alisema fedha hizo zinalenga kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii, kuboresha miundombinu pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi katika sekta mbalimbali.

Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 371.504 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikiwemo uendeshaji wa shughuli za Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi, huku Shilingi bilioni 132.90 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha,  Amos Makalla, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan ujenzi na matengenezo ya barabara.

Makalla aliwataka wabunge, wenyeviti wa halmashauri, madiwani pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushirikiana kwa karibu katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Akifungua Mkutano wa 51 wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha, Makalla aliwataka wataalamu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutumia zaidi mabaraza ya madiwani kama jukwaa la kupokea changamoto za barabara kutoka kwa wawakilishi wa wananchi.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuweka vipaumbele sahihi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara kulingana na mahitaji ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.

“Ni kupitia vikao kama hivi tunaweza kuazimia barabara zipi zipandishwe hadhi na zipi zijengwe kwa kiwango cha lami, kama ilivyoelekezwa kwa baadhi ya barabara muhimu katika Mkoa wa Arusha,” alisema Makalla.

Alitaja baadhi ya barabara zinazohitaji kupewa kipaumbele katika maboresho ya miundombinu kuwa ni pamoja na barabara ya kuingia Hospitali ya Wilaya ya Arusha DC, pamoja na barabara za Moshono–ByPass, Karatu–Eyasi na Longido–Siha, ambazo zina umuhimu mkubwa katika kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa.

Kwa mujibu wa Makalla, uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika maeneo hayo utachochea shughuli za kiuchumi, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuongeza kasi ya maendeleo ya Mkoa wa Arusha.

Katika kikao hicho pia, wajumbe walipokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa bajeti kutoka taasisi mbalimbali za miundombinu ikiwemo Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Taarifa hizo zilihusu utekelezaji wa bajeti kwa miaka ya fedha 2024/2025 na 2025/2026, huku kikao hicho pia kikijadili mpango kazi na bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka ujao wa fedha.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha Mkoa wa Arusha unaendelea kuimarisha miundombinu, kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi sambamba na utekelezaji wa agenda ya maendeleo ya Taifa.

Ends..

Post a Comment

0 Comments