MARTHA GIDO AWAHAMASISHA VIJANA KUJITOKEZA KUPIGA KURA OKTOBA 29
Mgombea ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Martha Gido, ametoa wito kwa vijana wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, akisema hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuchochea maendeleo na ustawi wa “Arusha mpya”.
Akizungumza jijini Arusha katika mkutano uliohusisha madereva wa bodaboda na bajaji zaidi ya 100, Marirta alisema ni jukumu la kila kijana kutumia haki yake ya kikatiba kwa kupiga kura na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayoamua mustakabali wa taifa.
“Kura yako ni sauti yako. Vijana tuna wajibu wa kujitokeza na pia kuhamasishana kuhusu umuhimu wa kuchagua viongozi wenye maono ya kweli ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema Martha
Akiweka msisitizo, alisema vijana wanapaswa kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta maendeleo ya kiuchumi, hasa katika Mkoa wa Arusha.
Alitolea mfano kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwemo mkopo wa Shilingi bilioni 200 uliotolewa kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi vijana wa Arusha Mjini.
“Ni wazi kila mmoja ameona matokeo ya uwezeshaji huu. Mkopo huo umeleta mafanikio makubwa kwa vijana, umefungua fursa mpya za biashara na kuboresha maisha ya wengi,” alisema.
Marirta aliongeza kuwa mikopo hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za serikali kuhakikisha vijana wanajengewa uwezo wa kiuchumi, hivyo ushiriki wao kwenye uchaguzi ni hatua ya kuendeleza mafanikio hayo.
Kwa upande wao, baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji walioshiriki mkutano huo walimpongeza Marirta kwa kuwapa mwamko wa kisiasa na kiuchumi, wakisema wana matumaini makubwa ya kuona Arusha ikiendelea kuwa mji salama wenye fursa nyingi za ajira na biashara kupitia sekta ya usafirishaji.
Dereva wa bodaboda kutoka Sombetini, John Richard, alisema ujumbe wa Marirta umewagusa vijana wengi kwa sababu unalenga katika kuwainua na kuwashirikisha kwenye maamuzi ya maendeleo.
“Tumezoea kuona wanasiasa wanakuja kutuahidi tu, lakini Marirta ametueleza mambo ya msingi yanayohusu maisha yetu moja kwa moja. Tutajitokeza kupiga kura kwa ajili ya mabadiliko chanya,” alisema John.
Naye dereva wa bajaji kutoka Mianzini, Saidi Ally, alisema vijana wanapaswa kutumia uchaguzi huu kama fursa ya kuchagua viongozi watakaosikiliza na kushughulikia changamoto zao.
“Tunataka viongozi wanaotupa nafasi ya kushiriki kwenye miradi ya maendeleo. Tumeona kazi ya Rais Samia kwenye miundombinu na mikopo, tunataka hayo yaendelee,” alisema Saidi.
Ends..



0 Comments