KESI YA VIGOGO WA BODABODA ARUSHA YAANGUKIA PUA -MLALAMIKAJI SAIPULANI RAMSEY AINGIA MITINI

Kesi ya Viongozi wa Bodaboda Yaangukia Pua – Mlalamikaji Ashindwa Kufika Mahakamani

Na Joseph Ngilisho— Arusha

Mahakama ya Mwanzo Themi, jijini Arusha, imelazimika kuifuta kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha (UBOJA), baada ya mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani kwa mara ya tatu mfululizo.

Kesi hiyo yenye namba 2015/2025, iliwahusisha viongozi watatu wa UBOJA akiwemo Mwenyekiti Okello Constantine, Katibu Hakimu Msemo, na Makamu Mwenyekiti Hemedi Mbaraka.

Uamuzi huo umetolewa leo oktoba 17 ,2025 na Hakimu Ndosi wa Mahakama hiyo, baada ya kuita kesi hiyo kwa mara ya tatu bila kufika kwa mlalamikaji aliyetajwa kwa jina la Saipulani Abubakary Ramsey.

Hakimu Ndosi alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria, kesi haiwezi kuendelea bila upande wa mlalamikaji kuwepo mahakamani, hivyo akaamua kuifuta rasmi na kuwaachia huru washtakiwa hao.

Awali, viongozi hao wa bodaboda walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 13 na 15, mwaka huu, bila mlalamikaji kufika, na leo kesi hiyo ilipoitwa kwa mara ya tatu bado alishindwa kujitokeza, jambo lililomlazimu Hakimu kutoa uamuzi huo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washtakiwa hao walidaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 7, 2025, majira ya saa 12 jioni katika ofisi za bodaboda eneo la Kaloleni jijini Arusha, ambapo aada ya kusomewa shtaka hilo walikana kosa  la kukabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 12 kutoka kwa Saipulani Abubakary Ramsey.

Fedha hizo zilidaiwa kutolewa kwa ajili ya kuwawezesha madereva wa bodaboda 2299 wa Jiji la Arusha kushiriki mapokezi ya mmoja wa wagombea aliyekuwa na ziara mkoani humo. Hata hivyo, ilidaiwa kuwa viongozi hao hawakutekeleza makubaliano hayo.

Washtakiwa hao walikamatwa Oktoba 7, 2025 na kushikiliwa mahabusu kwa takribani wiki moja bila dhamana hadi walipopandishwa kizimbani Oktoba 13, wakisomewa shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya mahakama kuifuta kesi hiyo leo, viongozi hao wa UBOJA wameachiwa huru, huku baadhi ya madereva wa bodaboda waliokuwepo mahakamani wakipongeza uamuzi huo na kuutaja kuwa “ushindi wa haki na ukweli.”

Akizungumza mara baada ya kutoka mahakamani, Mwenyekiti wa UBOJA, Okello Constantine, alisema wamevumilia mateso makubwa wakiwa mahabusu bila sababu za msingi na kwamba uamuzi huo ni ushahidi kuwa walisingiziwa.

> “Tumepitia kipindi kigumu sana. Tulifungwa kwa wiki nzima bila dhamana, bila ushahidi wowote. Tunashukuru mahakama kwa kutenda haki. Hii ni fundisho kwa watu wanaotumia majina ya bodaboda kuharibu taswira ya viongozi wake,” alisema Okello.


Naye Katibu wa umoja huo, Hakimu Msemo, alisema watarudi kazini mara moja kuendelea na majukumu ya kuwatetea madereva wa bodaboda wa Arusha.

> “Tutaendelea kufanya kazi zetu kwa uadilifu. Umoja huu ni wa watu maskini wanaotafuta riziki kwa jasho, si wa kuchezewa. Tunawaomba wanachama waendelee kuwa na imani na uongozi wao,” alisema.


Baadhi ya madereva wa bodaboda waliokuwepo mahakamani pia walitoa maoni yao, wakidai kuwa kesi hiyo ililenga kuharibu heshima ya viongozi wao.

> “Tulijua tangu mwanzo kuwa hawa viongozi hawana kosa. Tuliona ni njama za kisiasa na chuki binafsi. Tunamshukuru Mungu kwa haki kutendeka,” alisema dereva mmoja, Elia Mollel.


Dereva mwingine, Abbas Mwinuka, alisema tukio hilo limefungua macho ya madereva wengi kuhusu umuhimu wa umoja na mshikamano.

> “Leo tumejifunza kuwa tusikubali kugawanywa. Viongozi wetu wamekuwa mfano wa uvumilivu,” alisema.


Kesi hiyo sasa imefutwa rasmi, na viongozi wa UBOJA wamesema wataendelea kuimarisha umoja huo na kuhakikisha tasnia ya bodaboda mkoani Arusha inakuwa na nidhamu, uwazi, na ushirikiano na mamlaka zote za serikali.

-ends...

Post a Comment

0 Comments