JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAPIGA HATUA KUBWA KUDHIBITI FEDHA HARAMU

 JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAPIGA HATUA KUBWA KUDHIBITI FEDHA HARAMU

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA 

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) limeidhinisha hoja ya kumruhusu Mbunge Kennedy Aysason Mukulia kuwasilisha Mswada wa Sheria wa Kikanda wa Kuzuia Miamala ya Fedha Haramu (Illicit Financial Flows – IFFs), hatua inayotazamwa kama mwanzo wa mapinduzi makubwa katika kudhibiti upotevu wa fedha unaokwamisha maendeleo katika ukanda huo.

Uamuzi huo ulipitishwa baada ya hoja hiyo kuungwa mkono na Mhe. Godfrey Main, ambapo Bunge lilisisitiza umuhimu wa kuwa na sheria za pamoja zitakazosaidia Nchi Wanachama kupambana na tatizo hilo linaloikabili Afrika kwa kasi kubwa

Kupitia hoja hiyo, Bunge liliweka wazi kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 82(1) cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nchi Wanachama zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kifedha na sera za kiuchumi kwa lengo la kudumisha uthabiti wa kifedha, kukuza ujumuishaji wa kiuchumi na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa wananchi wake.

Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 83 cha Mkataba, pamoja na vifungu vya itifaki za Soko la Pamoja na Umoja wa Fedha, Nchi Wanachama zimeahidi kuratibu na kuoanisha sera zao za kiuchumi na kifedha ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kupitia mianya ya kifedha haramu.

🔹 Fedha haramu zatishia maendeleo ya ukanda

Bunge hilo la tano kupitia kikao chake cha nne , limeendelea leo Oktoba 7,2025 katika makao makuu ya EAC ,limetambua kuwa tatizo la mwamko wa fedha haramu (Illicit Financial Flows) ni tishio kubwa kwa maendeleo ya Nchi Wanachama na Bara zima la Afrika. 

Fedha hizo haramu zinatajwa kutokea kupitia njia kama ukwepaji kodi, uongo katika taarifa za biashara, bei za uhamishaji zisizo sahihi (transfer pricing), pamoja na biashara za kihalifu ikiwemo dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu, magendo na rushwa.

Wabunge walionyesha wasiwasi mkubwa kutokana na ongezeko la utegemezi wa Nchi Wanachama kwenye sekta ya madini na rasilimali asilia, hali inayowaweka katika mazingira hatarishi ya kupoteza mapato makubwa kupitia mianya hiyo ya kifedha haramu.


Katika hoja hiyo, wabunge walikubaliana kuwa juhudi za kudhibiti miamala ya fedha haramu lazima ziwe sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Miamala ya Fedha Haramu kutoka Afrika lililoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki.

Mapendekezo hayo yanajumuisha:

  1. Kuboresha utawala bora na uwajibikaji kwa kuhakikisha mikataba ya madini na biashara inakuwa wazi na yenye tija kwa nchi husika;
  2. Kuimarisha uwezo wa kisheria ili kuzuia na kudhibiti uhamishaji wa fedha haramu;
  3. Kuongeza nguvu na rasilimali kwa mamlaka za kodi na forodha;
  4. Kukuza ushirikiano wa kimataifa na uwazi katika taarifa za kodi, mauzo na faida za kampuni za madini;
  5. Kuoanisha sheria za kupambana na utakatishaji fedha na makubaliano ya kodi marudufu kati ya nchi wanachama.

🔹 “Ni jukumu letu la kisiasa,” asema Mukulia

Akizungumza baada ya hoja hiyo kupitishwa, Mhe. Kennedy Mukulia alisema, “Mapambano dhidi ya mtiririko wa fedha haramu ni jukumu letu la kisiasa na la kizalendo. Tukifanikiwa kudhibiti mianya hii, tutaimarisha uchumi wetu, kuongeza ajira na kuboresha mazingira ya biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.”

Aliongeza kuwa, utekelezaji wa hatua hizo utaimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika kukusanya mapato ya ndani, kupunguza utegemezi wa misaada, na kuongeza uwazi katika sekta binafsi.

Wabunge wengine walipongeza hatua hiyo, wakisema ni mwanzo wa safari muhimu ya kuhakikisha Jumuiya inasimama imara dhidi ya ufisadi wa kifedha na upotevu wa mapato.

“Tunapaswa kuwa na msimamo wa pamoja. Hakuna nchi itakayoweza kupambana na fedha haramu peke yake. Sheria za pamoja ndizo suluhisho,” alisema Mhe. Godfrey Main, aliyekuwa wa pili kuunga mkono hoja hiyo.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 64(5) ya Kanuni za Uendeshaji wa Bunge la EALA, hoja hiyo ilikuwa hatua ya kwanza ya kuruhusu Mbunge binafsi kuwasilisha mswada rasmi. Baada ya idhini hiyo, Mhe. Mukulia atawasilisha Mswada wa Sheria wa Kikanda wa Kuzuia Miamala ya Fedha Haramu, utakaojadiliwa na Bunge lote kabla ya kupitishwa na kupelekwa kwa Baraza la Mawaziri la Jumuiya kwa utekelezaji.


💬 “Kupambana na fedha haramu ni zaidi ya masuala ya kodi — ni kuhusu mustakabali wa uchumi wetu, utu wetu na maendeleo endelevu ya watu wa Afrika Mashariki,” alihitimisha Mukulia.

Ends..

Post a Comment

0 Comments