EWURA Yaadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Yaboresha Mfumo wa Leseni Mtandaoni
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kaskazini, imeadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kuwakaribisha wananchi kutembelea ofisi zake ili kupata majibu ya changamoto mbalimbali zinazohusu huduma za mafuta, gesi, nishati na maji.
Maadhimisho hayo, ambayo yalianza Oktoba 6, yamelenga kuimarisha mahusiano kati ya EWURA na wananchi, sambamba na kuongeza uelewa wa umma kuhusu haki na wajibu wao katika kupata huduma bora na salama.
Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Lorivii Long’idu, alisema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kupokea malalamiko na kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma hizo.
> “Tunatumia wiki hii kusikiliza changamoto za wananchi kama kuuziwa mafuta yasiyo na ubora, bei zisizo elekezwa, au gesi yenye ujazo pungufu. Pia tunatoa elimu kuhusu jinsi ya kutoa taarifa kwa EWURA ili hatua zichukuliwe kwa haraka,” alisema Long’idu.
Amebainisha kuwa EWURA kwa sasa imeanzisha mfumo mpya wa utoaji leseni kwa njia ya mtandao, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa vibali vya kuanzisha vituo vidogo vya mafuta na leseni kwa mafundi umeme, hususan katika maeneo ya pembezoni.
> “Tumelegeza baadhi ya masharti ili kuruhusu wajasiriamali wadogo kuanzisha vituo vya mafuta kwa gharama nafuu. Hii itasaidia kupunguza hatari ya kuuza mafuta kwenye vidumu majumbani, jambo ambalo ni hatari kwa afya na usalama wa wananchi,” aliongeza Long’idu.
Akizungumzia changamoto ya uuzaji wa gesi majumbani, alisema wananchi wanapaswa kuhakikisha gesi wanayonunua inapimwa kwenye mizani ili kuthibitisha ujazo sahihi, na iwapo watabaini udanganyifu, watoe taarifa kwa EWURA kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Bahati [jina kamili], alisema jukumu la mamlaka hiyo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye ubora unaostahili huku ikitoa elimu ya haki na wajibu kwa wateja.
> “Tunawahimiza wananchi kufika katika ofisi zetu kutoa maoni, kuuliza maswali na kutoa taarifa za changamoto wanazokutana nazo. Tupo hapa kusikiliza na kutatua migogoro kwa manufaa ya wote,” alisema Bahati.
Miongoni mwa wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, Bi. Rehema Shabani, mkazi wa Arusha, aliipongeza EWURA kwa kuandaa wiki hiyo akisema imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wengi .Alisema alikuwa na changamoto ya kuletewa ankara kubwa ya maji wakati huduma hiyo haipati kwa ufasaha ila anashukuru Ewura imesaidia kutatua kero hiyo.
> “Kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamikia baadhi ya vituo kuuza mafuta kwa bei tofauti, lakini kupitia elimu niliyoipata leo, nimejua namna sahihi ya kutoa taarifa kwa EWURA. Ni jambo jema kuona serikali inasikiliza wananchi moja kwa moja,” alisema Bi. Rehema.
Maadhimisho hayo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya EWURA ya kusogeza huduma karibu na wananchi, sambamba na kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ubora katika sekta za nishati na maji.
Mwisho.
0 Comments