ARUSHA YAADHIMISHA WIKI YA ELIMU YA WATU WAZIMA NJE YA MFUMO RASMI KWA KISHINDO,DC ATAKA HALMASHAURI KUTENGA FEDHA UJENZI WA MADARASA KILA KATA KWA AJILI YA ELIMU YA WATU WAZIMA,

 MGENI RASMI: HALMASHAURI ZITENGE FEDHA ZA UJENZI WA MADARASA KILA KATA KWA AJILI YA ELIMU YA WATU WAZIMA


Na Joseph   Ngilisho, Arusha


MAADHIMISHO ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yamefanyika leo katika viwanja vya Shule ya Msingi Levolosi, Wilaya ya Arusha Mjini, na kuhudhuriwa na mamia ya washiriki wakiwemo walimu, wanafunzi, wadau wa elimu pamoja na viongozi wa serikali.


Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni: “Kukuza Kisomo katika Dhama za Kidigitali kwa Maendeleo ya Taifa Letu”, ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa rika zote, hususan kwa watu waliokosa fursa ya kujiunga na mfumo rasmi wakiwa watoto.


Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini leo oktoba 4,2025, Afisa Tarafa jiji la Arusha,Chausiku Qaymo, aliitaka Halmashauri ya Jiji la Arusha kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika kila kata, ili kutoa fursa kwa watu waliokosa elimu kupitia mfumo rasmi kuweza kupata elimu hiyo.


“Serikali inatambua kuwa elimu ni haki ya kila raia bila kujali umri au changamoto zilizomkumba awali. Ujenzi wa madarasa ya elimu ya watu wazima katika kila kata utahakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kusoma na kuandika bila kikwazo chochote,” alisema Bi. Qaymo




Aidha, alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika elimu ni nguzo muhimu ya kuhakikisha wanafunzi wa rika zote, hususan waliokatiza masomo kwa changamoto kama ujauzito au hali ngumu za kifamilia, wanapata nafasi ya kuendelea na masomo yao kwa usawa.


Kwa sasa, Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imeanzisha darasa maalum la Sequip lenye wanafunzi 110, huku vituo vya elimu nje ya mfumo rasmi (MEMKWA) vikiwa 12 na jumla ya wanafunzi 315.


Awali, Afisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Arusha, Emmanuel Makundo, alisema sensa ya mwaka 2022 ilionyesha kuwa mkoa una kiwango cha asilimia 85 cha watu wazima wanaojua kusoma na kuandika, huku waliobakia asilimia 15 bado hawana ujuzi huo. Katika Wilaya ya Arusha pekee, idadi ya wasiojua kusoma ni asilimia 2.2 tu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt. Maduhu Nindwa, alibainisha kuwa jiji lina kiwango cha asilimia 98 cha watu wanaojua kusoma na kuandika, hali inayodhihirisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya elimu.


Katika hatua ya kuvutia, mwanafunzi mnufaika wa elimu hiyo, Jackline Sebastiani, alitoa ushuhuda wake akieleza jinsi alivyojikuta akikatisha masomo baada ya kupata ujauzito akiwa bado mdogo. Hata hivyo, alisema baada ya kujifungua alipata nafasi ya kurejea shuleni kupitia mpango wa elimu mbadala, hali iliyomsaidia kuendelea na safari yake ya kielimu.


“Nashukuru sana kwa utaratibu huu ulioanzishwa na serikali ya Rais Samia. Nilipoteza matumaini ya kusoma, lakini leo hii nimerudi shuleni na ninaendelea vizuri. Hii ni nafasi ya pili maishani mwangu na najua itaibadilisha familia yangu na jamii yangu,” alisema kwa hisia.


Maadhimisho hayo yalinogeshwa na burudani mbalimbali ikiwemo nyimbo za wanafunzi na muziki, hali iliyoongeza shamrashamra na hamasa kwa washiriki.


Aidha, wadau wa elimu walisisitiza kuwa elimu nje ya mfumo rasmi ni nyenzo muhimu ya kupunguza ujinga, kuongeza uelewa wa kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. 


Walisema kila mwaka kumekuwa na ongezeko la asilimia 7.5 la wanafunzi wanaojiunga na darasa la saba na kidato cha kwanza, ishara ya mwamko mpya wa elimu miongoni mwa wananchi.
















Ends.


Post a Comment

0 Comments