Joseph Ngilisho- Arusha
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wa chama hicho kuvunja makundi yaliyoibuka wakati wa mchujo wa ndani, na badala yake kushirikiana kwa umoja kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza katika Mkutano Maalum na wanachama wa CCM mkoani Arusha, uliowakutanisha viongozi wa chama, watia nia wa ubunge na udiwani, Wasira alisema ni wakati wa kuacha makundi na kuhamasisha kura kwa ajili ya ushindi halali, ikiwemo kwa wagombea waliopita bila kupingwa.
> “Makundi yavunjwe. Huu si muda wa kugawanyika. Hata kama mgombea wako hakuchaguliwa, muunge mkono aliyepewa nafasi. Kazi ya chama ni kuhakikisha kila mwanachama anashiriki kampeni ili chama kipate ushindi wa kishindo,” alisema Wasira.
Alisisitiza kuwa wagombea waliopitishwa bila ushindani hawapaswi kubweteka, bali wajitokeze kushiriki kikamilifu kwenye kampeni kwa kueleza ilani ya CCM kwa wananchi.
Katika hotuba yake, Wasira pia aligusia tabia ya baadhi ya watu wanaokibeza chama hicho kikongwe.
> “CCM ni chama chenye historia kubwa ya ukombozi na kimeendelea kusimamia maendeleo ya taifa. Hivyo mtu mmoja akisimama kukibeza chama hiki si jambo la kushangaza. Wapuuzeni, maana wenye historia na nguvu ya chama ni sisi wanachama,” alisema.
Aidha, alihimiza viongozi wa ngazi zote kuanzia matawi, mashina hadi mikoa, kushirikiana na wananchi kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Musa Matoroka, alisema hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ni shwari.
Alibainisha kuwa kati ya kata 160 za Mkoa wa Arusha, kata 119 zimepita bila kupingwa, huku kata 41 pekee zikishirikisha wagombea wa upinzani. Aidha, aliongeza kuwa katika Jimbo la Ngorongoro, mgombea wa CCM amepita bila mpinzani kuwania ubunge.
> “Kazi iliyobaki sasa ni kuhamasisha wanachama na wananchi kujitokeza kupiga kura ili CCM ipate ushindi wa halali,” alisema Makala.
> “Nawaomba wananchi wajitokeze kusikiliza sera za vyama vyote na kufanya maamuzi sahihi. Lakini jambo la msingi ni kudumisha amani, maana maendeleo hayatawezekana bila utulivu,” alisema Makalla.
ends.. .
0 Comments