BONANZA LA MICHEZO LA KUKATA NA SHOKA LALIPUA MLANGARINI
Na Joseph Ngilisho, Arumeru
Tamasha la michezo la kukata na shoka limeacha historia ya kipekee kata ya Mlangarini, wilayani Arumeru, baada ya timu ya Kiseriani kuibuka mabingwa kwa kuifunga Losirwai bao 2–1 kwenye mchezo wa fainali uliosisimua mashabiki na kuwatia moto mashujaa wa kijiji hicho.
Kiseriani waliibuka na zawadi ya shilingi 300,000 na kombe la ubingwa, huku Losirwai wakibeba shilingi 250,000 na kombe la pili. Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Manyire waliopata shilingi 200,000, na wenyeji Mlangarini wakamaliza nafasi ya nne kwa kuondoka na shilingi 150,000.
Bonanza hilo lililoandaliwa na mgombea udiwani wa CCM Kata ya Mlangarini, Emmanuel Mrema, liliwaleta pamoja mamia ya wananchi na kuibua msisimko mkubwa wa michezo, burudani na mshikamano wa kijamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mrema alisisitiza kuwa michezo si burudani pekee bali ni chachu ya maendeleo ya jamii.
“Kupitia michezo, vijana wetu wanapata nafasi ya kuonesha vipaji vyao, kuimarisha afya zao na kuachana na vishawishi vya maovu. Hii ni njia ya kuunganisha jamii na kuendeleza mshikamano,” alisema kwa hamasa.
Vijana walioshiriki walimpongeza Mrema kwa kusimamia maandalizi hayo, wakibainisha kuwa michezo imekuwa tiba ya changamoto nyingi zinazowakumba.
“Tamasha hili limetuondoa mitaani na limetuimarisha kiafya. Leo tunaamini tuna kiongozi anayetumia michezo kama chombo cha maendeleo,” alisema mmoja wa wachezaji wa Manyire.
“Diwani wetu anaona mbali. Ametuonyesha kuwa michezo ni shule ya nidhamu, mshikamano na heshima. Huu ni mwanzo mpya kwa vijana wa Mlangarini,” alisema huku akikabidhiwa kombe.
Mashabiki waliokuwa uwanjani walilipuka kwa nderemo na vifijo kila bao lilipoingia, huku muziki wa burudani zikiongeza joto la tamasha hilo.
Kwa ujumla, bonanza hilo limekuwa zaidi ya mashindano ya soka; limekuwa jukwaa la mshikamano na siasa za maendeleo, ambapo Mrema ameonekana kutengeneza dira ya kuwajenga vijana kupitia michezo, huku wananchi wakimuona kama kiongozi anayewekeza katika mustakabali wa kizazi kijacho.
Ends..
0 Comments