Wanafunzi Wawili Wadaiwa Kuzuiwa Kuondoka Shule ya Tengeru English Medium
By Arushadigital
Arumeru, Arusha – Taharuki imeibuka katika Shule ya Msingi Tengeru English Medium, iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha, baada ya wanafunzi wawili wanaodaiwa ada kuzuiwa kuondoka shuleni licha ya kumaliza mtihani na kuhitimu masomo yao ya darasa la saba.
Taarifa zinaeleza kuwa wanafunzi hao ni miongoni mwa wanafunzi 36 waliomaliza masomo yao Septemba 11, 2025, lakini uongozi wa shule uliwazuia kuondoka hadi pale wazazi wao watakapomalizia kulipa deni la ada.
Kwa mujibu wa chanzo cha karibu na shule hiyo, mmoja wa wanafunzi hao anadaiwa kiasi cha shilingi milioni 1 na laki 1, huku mwenzake akidaiwa shilingi laki 8.
> “Ni kweli watoto wapo shuleni, lakini sio kama wamefungwa, bali hawawezi kupewa kibali cha kuondoka kwa sababu ada bado haijalipwa. Hivyo wazazi wanaleta chakula chao hadi malipo yatakapokamilika,” kilieleza chanzo hicho.
Wanafunzi hao, ambao ni wa jinsia tofauti, wameripotiwa kuendelea kukaa shuleni huku wakiishi kwa msaada wa chakula kinacholetwa na wazazi wao kila siku.
Kauli za Wazazi
Mzazi wa mmoja wa wanafunzi waliodaiwa alionyesha masikitiko yake kuhusu hatua hiyo akisema:
> “Hatujakataa kulipa ada, ila changamoto za maisha zimekuwa kubwa. Tulitarajia shule ingetupa muda hadi tuwe tumekamilisha, lakini kitendo cha kumzuia mtoto kuondoka kinatufanya tuumie zaidi. Hawa watoto wanastahili furaha ya kuhitimu kama wenzao,” alisema mzazi huyo kwa sharti la kutotajwa jina.
Msimamo wa Serikali
Afisa Elimu wa Wilaya ya Arumeru, Bi. Neema Kivuyo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema ofisi yake imepokea malalamiko na inafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha haki za wanafunzi hazikiukwi.
> “Ni kweli tumepokea taarifa hizo, na tumewasiliana na uongozi wa shule. Ni wajibu wa wazazi kulipa ada, lakini pia ni wajibu wa shule kuhakikisha haki za watoto zinalindwa. Tutahakikisha panapatikana suluhu yenye maslahi kwa pande zote,” alisema Afisa Elimu huyo.
Mabadiliko ya Jina la Shule
Aidha, imebainika kuwa kwa sasa shule hiyo ipo katika mchakato wa kubadilishiwa jina, jambo ambalo limezua mjadala miongoni mwa jamii baada ya jina jipya kuonekana kwenye geti la shule hiyo.
Hata hivyo, uongozi wa shule hiyo bado haujatoa tamko rasmi kuhusiana na suala la kuzuiwa kwa wanafunzi pamoja na mchakato wa mabadiliko ya jina.
ends...
0 Comments