SABAYA AIBUKA AANGUSHA SHANGWE MKUTANO WA CCM,AMPA KIBARUA KIZITO DKT LUKUMAY

Sabaya Aibuka, Amuomba Lukumay Atatue Changamoto ya Vumbi , Ngaramtoni.

Na Joseph Ngilisho, Arumeru

ALIYEKUWA mtia nia wa ubunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ameibuka hadharani na kumuomba mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dkt. Johannes Lukumay, kuipa kipaumbele changamoto ya muda mrefu ya vumbi katika eneo la Ngaramtoni iwapo atachaguliwa.

Sabaya alitoa ombi hilo jana, Septemba 4, 2024, wakati wa mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa jimbo hilo.


Akiwa amepokelewa kwa shangwe kubwa na wanachama wa chama hicho, Sabaya alisema huu ulikuwa ni mkutano wake wa kwanza wa hadhara tangu amalize changamoto zilizokuwa zinamkabili wakati akiwa gerezani.

Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha mfumo wa sheria, hatua aliyoeleza imesaidia kupunguza mlundikano wa mahabusu katika gereza kuu la Kisongo, mkoani Arusha.

> “Nilipoingia gerezani nilikuta zaidi ya mahabusu 2,000, lakini nilipotoka walibaki 84 tu. Huu ni mpango mzuri wa Mama Samia wa kuweka sheria bora na kuhakikisha haki inatendeka,” alisema Sabaya huku akishangiliwa na wananchi.


Akiongea kwa kujiamini, Sabaya alisema ameamua kuungana na chama chake katika kumuunga mkono Dkt. Lukumay kwa sababu “CCM ni kubwa kuliko mtu mmoja.”

Sabaya alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Arumeru Magharibi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao na kuhakikisha wanakipa ushindi chama hicho ili kiendelee kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kushuhudiwa nchini.

Kwa upande wake, Dkt. Lukumay alimshukuru Sabaya kwa uungaji mkono na maoni yake, akiahidi kuyashughulikia kwa vitendo endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo.

“Nimepokea kwa heshima kubwa ushauri na maombi ya kijana wangu Sabaya. Ngaramtoni ni kitovu cha shughuli nyingi za biashara na kilimo, hivyo changamoto ya vumbi tutaitatua kwa kushirikiana na Serikali Kuu kupitia miradi ya barabara na mipango ya kimazingira. Lengo langu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na mazingira salama ya kuishi na kufanya shughuli zao,” alisema Dkt. Lukumay.


Mgombea huyo alisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa jibu la matatizo ya wananchi wa Arumeru kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi zote na kuwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao.

Ends....

Post a Comment

0 Comments