MPINA AIGARAGAZA INEC MAHAKAMANI, AREJESHWA KWENYE MCHAKATO WA URAIS

Mpina Aibwaga INEC, Arejeshwa Kwenye Mchakato wa Urais

By Arushadigital-Dodoma 

 

Aliyekuwa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, amepata ushindi mahakamani baada ya Mahakama Kuu, Masijala Kuu ya Dodoma, kumrejesha rasmi kwenye mchakato wa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo.


Uamuzi huo ulitolewa leo Alhamis , September 11,2025 baada ya jopo la majaji watatu,Abdi Kagomba ,Evaristo Longopa na John Kahyoza, kupinga hatua ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iliyokuwa imebatilisha uteuzi wake kwa madai ya kutokidhi vigezo vya kikatiba na kisheria.


Katika hukumu hiyo, mahakama ilieleza kuwa sababu zilizotolewa na INEC hazikuwa na mashiko ya kisheria na hivyo kumzuia mgombea kuendelea na safari ya kisiasa kulikuwa ni kinyume cha haki za msingi za kidemokrasia.


“Mahakama hii inatengua uamuzi wa INEC na kumrejesha Bw. Luhaga Mpina kama mgombea halali wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” ilisomeka sehemu ya hukumu hiyo.


Awali INEC ilimtangaza Mpina kuondolewa kwenye orodha ya wagombea urais mwishoni mwa mwezi uliopita kwa maelezo kuwa hakukidhi matakwa ya kikatiba. Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa katika nyanja za kisiasa na kisheria, huku ACT-Wazalendo ikiahidi kupigania haki ya mgombea wao


Katibu Mkuu wa chama hicho alisema:

“Uamuzi huu ni ushindi si tu kwa chama chetu bali kwa demokrasia ya Tanzania. Ni ishara kwamba haki inapiganiwa na mahakama zetu zinaweza kusimama kwa ujasiri.”

Akizungumza mara baada ya hukumu, Mpina alisema hatua hiyo imempa nguvu mpya kuendelea na kampeni zake.

“Nimekuwa nikiamini katika mchakato wa kisheria, na sasa naona haki imetendeka. Nawaahidi Watanzania kuwa nitapigania ajenda za maendeleo, umoja na uwajibikaji,” alisema kwa msisitizo huku akishangiliwa na wafuasi wake.


Kwa kurejeshwa kwake, Mpina sasa atashiriki rasmi katika mchakato wa kampeni za urais ndani ya ACT-Wazalendo na hatimaye kuwania nafasi ya juu zaidi ya uongozi wa taifa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Ends..


Post a Comment

0 Comments