By Arushadigital
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ameiomba kesi ya Uhaini inayomkabili irushwe mubashara ili kuondoa tatizo la wafuasi wa chama hicho kupigwa nje ya Mahakama, wafuatilie huko waliko.
Aidha, amekataa upande wa Jamhuri kumuita mwenzetu, kwa sababu yeye siyo mwenzao na kutaka wamuite mshtakiwa kutokana na kesi ya jinai ya Uhaini inayomkabili.
Ombi hilo amelitoa leo mbele ya Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidizana na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde kabla ya upande wa Jamhuri kujibu hoja za pingamizi lake kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka na maelezo ya mashahidi.
"Waheshimiwa majaji na mimi kwa upande wangu nipo tayari kuendelea, lakini kabla ya kuendelea kuna mambo mawili nataka niyazungumze ambapo moja mnaweza kuliona ni dogo ila kwangu ni kubwa," alidai Lissu
Lissu alidai kuwa kuna ombi ameandika kwa Msajili wa Mahakama tangu Septemba 4, 2025 hadi leo Septemba 18,2025 ni wiki ya pili tangu ameandika na kwa madai kwamba hajajibiwa.
"Waheshimiwa majaji mlisema suala hili mtalitoa ufafanuzi, hamjalitolea hadi leo, pamoja na kwamba nipo ndani gerezani lakini nafuatilia watu wanavyopigwa hapo nje, taarifa zimesambaa dunia inajua,"
"Ili kuondokana na tatizo hili ni kuyatangaza mashauri haya live ili wasije mahakamani kufuatilia ili watu wasipigwe na mapolisi hili jambo halina afya yoyote kwa kinachoendelea katika nchi hii," alidai Lissu
Katika suala la kuitwa mwenzetu, Lissu alidai kuwa mara kadhaa Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga amekuwa akimuita mwenzetu, yeye siyo mwenzao anataka kuitwa mshtakiwa kwa sababu anakabiliwa na kesi ya jinai ya Uhaini.
"Wakili Katuga amekuwa akiniita mwenzetu mwenzetu mara kwa mara siyo leo tu, mimi namwambia siyo mwenzao aniite mshtakiwa,"alidai Lissu
Baada ya kudai hayo, Jaji Ndunguru alimueleza Wakili Katuga kuwa mshtakiwa asingependa kuitwa mwenzetu, kwa hiyo anataka kuitwa kwenye nafasi yake ya mshtakiwa.
"Kwa sababu Mahakama imeshatoa muongozo tumelipokea kama alivyosema tutamuita mshtakiwa, lakini kwa ufafanuzi kidogo nilisema mwenzetu kwa sababu yeye mwenyewe alisema kuwa amedumu kwenye sheria miaka 20 na sisi huwa kuna majina tutaitana hivyo ndiyo maana nikamuita mwenzetu, sikumaanisha yupo upande wetu,"alidai Wakili Katuga
Pia, Wakili Katuga alidai anamuita mwenzetu kwa sababu ni sehemu ya kwenye kesi, bila yeye wao hawapo na bila wao yeye hayupo.
"Hili lingine lipo ndani ya mamlaka ya Mahakama tutalitolea maelekezo," alisema Jaji Ndunguru kuhusu ombi la Lissu la kurushwa kesi mubashara
Katika kesi hiyo inadaiwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam mshtakiwa Lissu akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alitangeneza nia ya kushawishi au kuchochea umma ya kuweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania kwa kusema maneno yafuatayo
"Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko....kwa hiyo tunaenda kukinukisha sanasana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana,".
0 Comments