JIJI LA ARUSHA LATENGA BILIONI 11.9 KUKOPESHA WANAWAKE VIJANA NA WALEMAVU

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

HALMASHAURI ya Jiji la Arusha imetenga jumla ya shilingi bilioni 11.9 kwa ajili ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza leo jumanne septemba 23,2015 jijini Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alisema fedha hizo ni nyenzo muhimu kwa wajasiriamali wadogo kujikwamua kiuchumi na kusisitiza kuwa mikopo hiyo ni ya wananchi na si mali ya watumishi wa serikali.

> “Tunasisitiza vigezo vya uombaji vizingatiwe ipasavyo ili kila mhusika anufaike. Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata mitaji ya kujiendeleza na si vinginevyo,” alisema Mkude.


Onyo kwa wahujumu miundombinu

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya alitoa onyo kali kwa wananchi wanaohujumu miundombinu ya taa za barabarani na barabara, akibainisha kuwa kitendo hicho kinasababisha hasara kubwa kwa serikali na kudumaza maendeleo.

> “Mtu yeyote atakayebainika kuiba au kuharibu taa za barabarani atachukuliwa hatua kali za kisheria. Nimeweka zawadi ya shilingi 500,000 kwa atakayetoa taarifa za uhakika kuhusu waharifu hao,” alisisitiza.


Mkude aliongeza kuwa jukumu la kulinda miundombinu si la serikali pekee bali la kila mwananchi, ili kuhakikisha uwekezaji wa umma unawanufaisha wote.

Miradi ya maji na barabara

Aidha, alieleza kuwa zaidi ya wananchi 21,000 wa Kata ya Baraa watanufaika na mradi mkubwa wa maji safi unaoendelea kutekelezwa, lengo likiwa kuondoa kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji salama jijini Arusha.

Pamoja na hilo, serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za ndani kwa kiwango cha lami, hatua itakayorahisisha usafiri na kurahisisha shughuli za kiuchumi, huku wananchi wakihimizwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Kauli ya wananchi

Mkazi wa Kata ya Baraa, Neema Richard, alisema hatua hiyo ni uthibitisho kwamba serikali inaguswa na maisha ya wananchi wa kawaida.

> “Mimi ni mama mjane, ninafanya biashara ndogo ya mboga. Nikifanikiwa kupata mkopo huu itakuwa mwanga mkubwa kwangu na watoto wangu. Lakini pia mradi wa maji na barabara utaokoa muda tuliokuwa tunapoteza kila siku. Hii ni faraja kubwa kwa wananchi wa kawaida,” alisema Neema kwa furaha.


Angalizo kwa madalali

Katika mkutano huo, Mkude aliwakumbusha pia madalali mkoani Arusha kufuata taratibu kabla ya kukamata mali za wadaiwa, akisisitiza kuwa njia pekee ya kumaliza deni ni kulipa.

> “Dawa ya deni ni kulipa. Hata hivyo, taratibu lazima zifuatwe ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima,” alionya.


Mkuu huyo alibainisha kuwa motisha ya zawadi ya fedha taslimu itatolewa kwa wananchi wote watakaoshirikiana na serikali katika kufanikisha kuwabaini wahalifu na kuimarisha ulinzi wa mali za umma.

-Ends...

Post a Comment

0 Comments