TAHARUKI ,NDEGE AINA YA BOMBARDIER YAKATAA KUWAKA UWANJA WA NDEGE KISONGO ARUSHA,YAVUTWA NA KUPELEKWA KARAKANA.

 NDEGE AINA YA BOMBARDIER YAKATAA KUWAKA UWANJA WA NDEGE KISONGO ARUSHA

By Arushadigital

Taharuki imetanda katika Uwanja wa Ndege wa Arusha uliopo Kisongo, baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Dash 8 Q400 kushindwa kuwaka mapema leo asubuhi,Asosti 7,2025 hali iliyosababisha usumbufu kwa abiria waliokuwa wakielekea Dar es Salaam.


Tukio hilo limetokea majira ya saa 2:30 asubuhi, ambapo ndege hiyo iliyotarajiwa kuruka kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), iligoma kuwaka mara baada ya marubani kuanza maandalizi ya kuondoka.


Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa abiria walikuwa tayari wamepanda ndege hiyo, lakini ghafla walitaarifiwa kuwa kuna hitilafu ya kiufundi iliyohitaji ukaguzi wa wahandisi kabla ya kuendelea na safari.


“Tulishaingia ndani ya ndege tukisubiri kuondoka, lakini baada ya muda tukatangaziwa kuwa kuna changamoto ya kiufundi. Baadaye tukaambiwa tushuke,” amesema mmoja wa abiria waliokuwa kwenye safari hiyo.


Wataalamu wa ufundi kutoka shirika hilo la ATCL wakitokea Jijini Dar es Salaam walifika haraka eneo la tukio na kuanza ukaguzi wa ndege hiyo, ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa matatizo yalikuwa katika mfumo wa kuwasha injini ,hata hivyo baada ya marekebisho hayo ndege hiyo ilifanikiwa kuondoka katika uwanja huo. 


Msemaji wa ATCL, Sarah Gady alisema hana taarifa juu ya tukio hilo na alipotakiwa kutoa ufafanuzi kwa kile kilichotokea baada ya abiria kushushwa ndani ya ndege na kupelekwa eneo ya kusubiria abiria, alikata simu na kutopokea tena.


Wakati ndege hiyo ikihitaji ukarabati, baadhi ya abiria walielekezwa kwenye usafiri mbadala huku wengine wakitaarifiwa kuhusu mabadiliko ya ratiba.


Hadi kufikia saa 5 , juhudi za kurekebisha tatizo hilo zilikuwa zikiendelea, huku uongozi wa uwanja huo ukihakikishia umma kuwa shughuli nyingine za ndege zinaendelea kama kawaida.


Tukio hili limeibua mijadala kuhusu uimara wa ndege zinazotumiwa na shirika hilo la taifa, japo wataalamu wanasema ni jambo la kawaida kwa ndege yoyote duniani kukumbwa na hitilafu ndogondogo za kiufundi, hivyo siyo lazima kuwa na hofu.


Ndege ya Bombardier Q400 ikiwa imesimama uwanjani.


Post a Comment

0 Comments