MSHAURI WA RAIS SOPHIA MJEMA AONGOZA MAMIA YA WAUMINI TWARIQA KUOMBA DUA KUMWOMBEA RAIS SAMIA NA TAIFA ,AADHIMISHA KUMBUKIZI KIFO CHA SHEIKH DARUWESHI ARUSHA.

MSHAURI WA RAIS SOHIA MJEMA AONGOZA DUA KULIOMBEA TAIFA ARHSBA 

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 


MSHAURI wa Rais katika Masuala ya wanawake na Makundi Maalumu , Sophia Mjema, ameongoza mamia ya waumini wa taasisi ya Twariqa, Zawia Kuu jijini Arusha katika dua maalumu ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na kuombea amani ya Taifa, kuelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.

Dua hiyo imefanyika leo agosti 23,2025 katika viwanja vya taasisi hiyo Zawia Kuu Arusha, ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Kiongozi Mkuu wa Taasisi ya Twariqa nchini, Sheikh Salim Daruweshi, aliyefariki dunia Agosti 12,2024 Mwaka jana.

 Tukio hilo limehudhuriwa na mamia ya  waumini kutoka mikoa mbalimbali nchini,waliokesha kuomba dua, likiwa limejaa mshikamano na mshangao wa kiroho 

Akizungumza leo agosti 23,2025 katika maadhimisho hayo,  Mjema alisema dua hiyo ina umuhimu mkubwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kwani inalenga kudumisha mshikikano wa kitaifa na kuimarisha hali ya amani ambayo ndiyo nguzo ya maendeleo ya Taifa.


“Nchi yoyote inapofikia kipindi cha uchaguzi huwa inakabiliwa na changamoto za kijamii na kisiasa, ndiyo maana dua kama hii ni ngao ya kulinda utulivu. Tunamuombea Rais wetu Mama Samia pamoja na Taifa lote ili Mungu atuwezeshe kupita salama katika kipindi hiki muhimu,” alisema.




Katika hotuba yake, Mjema pamoja na kuwashukuru waumini kwa dua ya kuliombea taifa,pia aliwahimiza wanawake wa Kiislamu kutumia fursa za vikundi vya ujasiriamali ili kuimarisha uchumi wao binafsi na wa familia. 


Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatilia mkazo mikopo na uwezeshaji wa kiuchumi, hivyo wanawake wanapaswa kuunda vikundi rasmi vitakavyowawezesha kupata mitaji kutoka serikalini.


“Wanawake wa Kiislamu mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kujitegemea kimaisha. Serikali ipo tayari kuwaunga mkono kupitia mikopo ya maendeleo, hivyo mjipange kwa kuunda vikundi ili msikose nafasi hii muhimu,” alisisitiza.


Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa dua na mawaidha kutoka kwa viongozi wa dini hiyo waliomzunguka Sheikh Salim Daruweshi enzi za uhai wake, wakisisitiza juu ya kuendeleza urithi wake wa kusimamia misingi ya upendo, mshikamano na utulivu katika jamii.


Waumini waliohudhuria walionekana kuguswa na mafunzo hayo, huku wakieleza kuwa kumbukumbu ya Sheikh Daruweshi imeendelea kuwa mwongozo wa kiroho na dira ya kudumisha mshikikano wa Waislamu nchini.


Dua hiyo ya kiroho ilitanguliwa na mkesha wa amani katika makao makuu ya Taasisi hiyo na imebeba ujumbe mpana wa kitaifa: kwamba amani, mshikamano na mshirikiano ni msingi muhimu wa maendeleo, na kwamba kila raia ana wajibu wa kuchangia kudumisha hali hiyo kuelekea uchaguzi mkuu na hata baada ya uchaguzi.











Ends..

Post a Comment

0 Comments