LUKUMAY AANDIKA HISTORIA ARUMERU MAGHARIBI, AANGUSHA SHEREHE NZITO YA KUWASHUKURU WAJUMBE LICHA YA JINA KUTORUDI,ALIYETEULIWA AIBUKA KATIKATI YA SHEREHE

LUKUMAYE AANDIKA HISTORIA ARUMERU, AANGUSHA SHEREHE NZITO YA SHUKRANI LICHA YA JINA KUTORUDI

Na Joseph Ngilisho- ARUMERU 


Aliyekuwa mtia nia wa ubunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elias Lukumaye, ameushangaza umma baada ya kuandaa sherehe kubwa ya kuwashukuru wajumbe na wananchi wa jimbo hilo licha ya jina lake kutoorodheshwa katika mchakato wa mwisho wa uteuzi wa wagombea.


Akizungumza nyumbani kwake mbele ya mamia ya wananchi na waandishi wa habari leo Agosti 24,2025, Lukumay alisema ameona ni busara kuonyesha shukrani kwa upendo na mshikamano aliopata kutoka kwa wananchi wa Arumeru Magharibi wakati alipokuwa ameonesha nia ya kugombea ubunge.

> “Mahaba haya na mapenzi mliyoyaonyesha juu yangu, sina cha kuwalipa. Mlinipa ushirikiano mkubwa lakini kwa bahati mbaya jina langu halikurudi. Nimeona niwashukuru kwa kujumuika pamoja nami leo,” alisema Lukumaye.

Ameongeza kuwa malengo yake hayakuwa tu kupata ubunge, bali kusaidia wananchi kushughulikia changamoto zinazowakabili katika kata 27 za jimbo hilo.

> “Sisi jambo letu halikuwa ni kupata ubunge pekee, bali kuhangaika na shida za wananchi wa Arumeru Magharibi. Naamini bado tutaendelea kushirikiana na mbunge atakayechaguliwa ili kuleta maendeleo,” alisema.



Hafla Yazua Shamrashamra

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge mteule wa jimbo hilo kupitia CCM, Johannes Lukumay, wenyeviti wa mitaa, mabalozi, madiwani wateule na wale waliomaliza muda wao, pamoja na wananchi kutoka kata mbalimbali.


Kwa upande wake, Mbunge mteule Johannes Lukumay aliwashukuru wananchi kwa kumwamini na kumpa kura za kishindo na kuahidi kupambana na umasikini, huku akitoa kipaumbele kwa sekta ya elimu.


> “Nilipokuwa nasoma shule ya msingi nilitembea bila viatu kwa miaka saba. Niliweza kuvaa viatu nilipofika sekondari, ndiyo maana nachukia umasikini. Kwa sasa nasomesha watoto 89 wasio na uwezo wa kununua hata daftari na kalamu. Nimepania kuondoa umasikini kwa kuanzisha mfuko maalumu wa elimu kupitia wafadhili ili kuhakikisha kila mtoto wa Arumeru anapata nafasi ya kusoma bila kikwazo cha ada,” alisema Lukumay.


Aliongeza kuwa jukumu kubwa la uongozi ni kuunganisha wananchi na kuondoa makundi ya kifrakta ili mshikamano wa kisiasa uwe chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika jimbo hilo.









Ends....

Post a Comment

0 Comments