By Arushadigital, Zanzibar
Chama cha ACT-Wazalendo kimezindua rasmi kampeni zake kwa kumtambulisha Luhaga Mpina kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Othman Masoud Othman kuwa mgombea urais wa Zanzibar, katika mkutano uliofurika maelfu ya wafuasi katika viwanja vya Michenzani, Unguja.
Uzinduzi huo uliofanyika jana umeashiria mwanzo wa mbio za urais kwa chama hicho, huku viongozi wakuu wakitoa hotuba zenye hamasa na matumaini mapya kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Akihutubia umati huo, Mpina aliwataka Watanzania kuungana katika kuleta mabadiliko, akiahidi kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote.
“Tunakuja kurejesha heshima, haki na uwiano wa kugawana utajiri wa taifa. Hizi damu za mabadiliko mnazoziona ni zile zile zilizopiganwa na mashujaa wetu wa demokrasia,” alisema Mpina, akimkumbuka marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kama nguzo ya mapambano ya kisiasa visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake, Othman Masoud, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, alisisitiza kuwa kampeni zao zitaweka mbele maslahi ya wananchi badala ya tamaa za madaraka.
“Tunapigania Zanzibar yenye heshima, yenye uhuru wa kweli na usawa kwa wote. Hatuji hapa kwa ajili ya vyeo, bali kwa ajili ya kusuluhisha changamoto zinazowakabili Wazanzibari,” alisema.
Kabla ya uzinduzi huo, Halmashauri Kuu ya Taifa ya ACT-Wazalendo ilimthibitisha Mpina kwa kura 559 kati ya kura 606 zilizopigwa (sawa na asilimia 92.3) na kumpitisha Othman kwa kura 606 sawa na asilimia 99.5 ya kura zote.
Mkutano huo wa hadhara ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa chama hicho, wabunge, wawakilishi wa vyama rafiki, pamoja na wanachama kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.
ACT-Wazalendo imeeleza kuwa kampeni rasmi zitazinduliwa wiki chache zijazo, zikilenga kujenga umoja wa kitaifa, kuimarisha uchumi wa wananchi wa kipato cha chini, na kuondoa dhuluma katika ugawaji wa rasilimali.
Ends...
0 Comments