MNYETI AKALIA KUTI KAVU UBUNGE MISUNGWI, TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAMKAANGA MBAYA,AWEKEWA PINGAMIZI LA KUTOGOMBEA UBUNGE TUHUMA ZAKE ZAFIKISHWA KWA KATIBU MKUU CCM. DKT KIBOLA AMKALIA KOONI!


*Tume ya Haki za Binadamu Yamchongea Mnyeti na Mtendaji wa Kata: Yawasilisha Taarifa ya Matumizi Mabaya ya Madaraka

By arushadigtal 


TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa ripoti nzito ya uchunguzi dhidi ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, pamoja na aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Emboreet wilayani Simanjiro,  Belinda Sumari, wakituhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na ukiukaji wa haki za binadamu.


Taarifa hiyo ya uchunguzi iliyokamilika Oktoba 25, 2021, ilitolewa rasmi na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, na kueleza kwa kina namna viongozi hao walivyokiuka sheria na taratibu wakati wa kushughulikia mgogoro wa kitalu cha uwindaji kilichopo Pori Tengefu la Simanjiro.


Mlalamikaji mkuu katika sakata hilo ni Dk. Hamis Kibola, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya HSK Safaris Ltd – inayomiliki kitalu halali cha uwindaji katika eneo hilo. Dk. Kibola alidai kuwa alizuiwa kuingia katika kitalu chake licha ya kuwa na vibali halali, kisha kukamatwa tarehe 26 Juni 2020 na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Orkesumet pasipo kufikishwa mahakamani.


Tume imebaini kuwa hatua hiyo ya kumkamata ilifanywa na viongozi hao kwa kutumia mamlaka yao kinyume cha sheria, jambo lililotafsiriwa kuwa ni ukiukwaji wa haki ya uhuru binafsi, haki ya kumiliki mali na haki ya kufanya kazi kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Tume, Mnyeti aliunda kamati isiyo halali kwa mujibu wa sheria, kisha kuitumia kumdhibiti Dk. Kibola kuingia katika eneo lake la biashara. Vilevile, alidai kupokea barua kutoka kwa wananchi wakilalamikia shughuli za uwindaji, lakini uchunguzi wa Tume haukupata ushahidi wowote wa kuwepo kwa barua hizo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo:

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ichukue hatua stahiki za kisheria kutokana na ukiukwaji uliofanywa.


Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) ifanye uchunguzi kuhusu uwepo wa shughuli za uwindaji haramu katika Pori Tengefu la Simanjiro Magharibi.


Viongozi hao wawajibishwe kwa mujibu wa sheria kutokana na matumizi mabaya ya madaraka.

Ripoti hii ni ushahidi kwamba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inasimama kama nguzo muhimu ya ulinzi wa haki za Watanzania dhidi ya viongozi wanaotumia mamlaka vibaya. 


Hatua hii pia inatoa fursa ya kujadili kwa kina namna ambavyo uwajibikaji unapaswa kuimarishwa serikalini ili kuepuka matukio kama haya siku zijazo.






Post a Comment

0 Comments