By arushadigtal
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Upelelezi wa Masuala ya Fedha nchini Equatorial Guinea, Baltasar Engonga, anakabiliwa na kifungo cha miaka 18 jela baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Malabo, kwa kesi ya ufisadi.
Engonga amekuwa rumande katika Gereza la Black Beach, tangu Septemba 2024, kutokana na uchunguzi wa ufisadi, tofauti na sakata la kanda zaidi ya 400 za ngono zilizokutwa ofisini na nyumbani kwake, zikihusisha wanawake mashuhuri.
Anakabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu wa fedha akiwa pamoja na maofisa wengine waandamizi wa zamani.
Wakati wa kesi hiyo Jumatatu, waendesha mashtaka wameeleza kile walichokiita mpango wa hali ya juu wa kutapeli fedha za umma kwa manufaa binafsi.
Mpango huo unadaiwa kuongozwa na Engonga, alipokuwa Mkuu wa Kurugenzi ya Bima na Bima Ndogo kati ya mwaka 2015 hadi 2020.
Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao wa Le Bled Parle, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Taifa amependekeza adhabu kali, miaka nane kwa kosa la ubadhirifu wa fedha za umma, miaka minne na miezi mitano kwa kujipatia mali isivyo halali, na miaka sita na siku moja, kwa matumizi mabaya ya madaraka.
Mbali na adhabu ya kifungo, Engonga anakabiliwa pia na faini ya zaidi ya faranga CFA milioni 910 (takriban dola milioni 1.5 za Marekani) pamoja na marufuku ya kushika nyadhifa yoyote ya umma kipindi chote cha kifungo.
Mtaalamu huyo wa uchumi mwenye umri wa miaka 54 siye pekee anayekabiliwa na kesi hiyo. Maofisa wengine sita waandamizi wa zamani wa serikali nao wanashitakiwa.
Wengine wanaokabiliwa na kesi ni pamoja na Carmelo Julio Matogo Ndong, Ireneo Mangue Monsuy Afana, na Florentina Iganga Iñandji, wanaoshitakiwa kwa madai ya ubadhirifu wa fedha za umma, katika kile mamlaka zinachoeleza kuwa ni mtandao mpana wa ufisadi wa kifedha.
Kesi hiyo inatarajiwa kudumu kwa siku tatu, huku utetezi ukiendelea kutolewa na mawakili wa washitakiwa wiki hii.
Kumbuka kuwa wakati wa uchunguzi wa kesi hiyo ya udanganyifu, Engonga anadaiwa kukutwa na kanda zaidi ya 400 za ngono zikihusisha wake wa watu mashuhuri nchini humo.
Msako wa ghafla uliofanywa na maofisa wa ANIF nyumbani na ofisini kwake, ulisababisha kukutwa kwa CD kadhaa zilizofichua vitendo vyake vya kingono na wake wa watu mbalimbali walioko kwenye nafasi za juu serikalini.
Video hizo zinadaiwa kuonyesha mahusiano ya kingono na watu mashuhuri, wakiwamo mke wa kaka yake, binamu yake, dada wa Rais wa Equatorial Guinea, mke wa Mkurugenzi Mkuu wa Polisi, pamoja na wake wa mawaziri takriban 20 wa nchi hiyo, miongoni mwa wengine.
Chanzo: PUNCH
0 Comments