By arushadigtal-Dar
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa agizo jipya linalowazuia viongozi wa serikali na kisiasa kupewa nafasi ya kuzungumza au kusalimia mbele ya madhabahu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu.
Kwa mujibu wa agizo hilo, hata kama Misa itahudhuriwa Rais, Waziri, Mbunge au kiongozi mwingine wa kisiasa, kiongozi wa ibada (iwe ni Padre au Askofu) atatambua uwepo wake kwa heshima bila kumpa nafasi yoyote ya kuongea, kutoa hotuba au hata salamu.
Baraza hilo limeeleza kuwa madhabahu ni mahali patakatifu pa Ibada, na si jukwaa la kisiasa au majukwaa ya kiraia. Hivyo, uamuzi huo unalenga kulinda utakatifu wa liturujia na kuepusha mchanganyiko kati ya imani na siasa.
Aidha, endapo kiongozi huyo wa serikali au kisiasa atakuwa na sadaka au ujumbe wa shukrani, shukrani hizo zitatolewa kwa niaba yake na Katekista, Padre au Askofu anayeongoza ibada.
Agizo hili linakuja wakati ambapo katika baadhi ya maeneo viongozi wa kisiasa wamekuwa wakipewa nafasi ya kuzungumza ndani ya makanisa wakati wa Ibada, jambo ambalo limekuwa likileta mjadala miongoni mwa waumini.
TEC imesisitiza kuwa Kanisa Katoliki litaendelea kuwakaribisha viongozi wote wa serikali na kisiasa kama waumini, lakini nafasi yao katika Ibada itakuwa sawa na waumini wengine.
0 Comments