Na Joseph Ngilisho- MONDULI
SHULE ya Sekondari ya Tumaini Senior iliyopo Makuyuni wilaya ya Monduli, Mkoani Arusha imejiwekea mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha nne na sita katika shule hiyo wote wanafaulu vizuri.
Akiongea wakati wa mahafali ya nne ya kidato cha sita yaliyofanyika leo Mei,23,2025 shuleni hapo,Mkurugenzi wa shule hiyo , Modest Bayo alisema kuwa mkakati mojawapo ni pamoja na kuhakikisha walimu wanaongeza morari wa kufundisha ,kuwekeza zaidi katika maabara za kujifunzia kwa ajili ya masomo ya sayansi pamoja na elimu ya kujitegemea kwa ajili ya wanafunzi kujiendeleza inayotolewa shuleni hapo.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri na sasa wanauhakika wa kufanya vizuri kwa wanafunzi wote wanaohitimu shuleni hapo.
"Shule yetu imekuwa ikifanya vizuri tangu miaka ya nyuma hata hawa wanaohitimu leo tunauhakika watafanya vizuri zaidi,na katika elimu ya sayansi na Teknologia tumehakikisha tunakuwa na kila aina ya maabara ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi na maarifa na elimu ya kujitegemea"
Bayo aliwakaribisha wazazi kwenda kuwekeza watoto wao katika shule hiyo ili wanufaike na msingi wa elimu bora inayotolewa katika mazingira salama na ya kiroho.
Alitoa rai kwa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujilinda na magonjwa mbalimbali na kutokubali kurubuniwa na watu wasio na nia njema kwani serikali na wazazi wamewekeza katika elimu hivyo kwa kiasi kikubwa.
Awali mdau wa elimu wa shule hiyo kutoka nchini Marekani,Kellie Lala alizitaka shule za sekondari kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi ili kuzalisha ubunifu kwa maendeleo ya Taifa.
Akiongea katika mahafali hayo akiwa mgeni rasmi alisema katika kipindi cha miaka ishirini aliyofahamiana na Mkurugezi wa shule hiyo amefurahishwa na namna shule hiyo inavyotoa kipaumbelea kwa watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi
"Najisikia vizuri kuendelea kusapoti elimu katika shule ya sekondari Tumaini ,ndoto ya Bayo imekuwa ndoto yangu"
Kellie aliwaasa wahitimu kuhakikisha wanazingatia yale yote waliyojifunza na kuendela kujiamini ,kuzingatia maadili , Upendo na uaminifu.
Aliwataka elimu walioipata iwasaidie kuboresha maisha yao na Taifa kwa ujumla wasiishie hapo bali iwe mwanzo wa kujiendeleza zaidi.
Naye mkuu wa shule ya sekondari,Tumaini Senior ,Sifael Msengi alisema kuwa mahafali hayo ni ya nne tangu kuanzishwa kwa shule hiyo na wamekuwa wakifanya vizuri sana katika awamu zote nne.
Alifafanua kuwa shule hiyo imejikita zaidi katika masomo ya biashara na sayansi jamii na kwamba mwaka jana 2024 jumla ya wahitimu walikuwa 53 kati yao 40 walipata divisheni 1 na waliobaki walipata divisheni 2.
Alisema mpango mkakati wao ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaohitimu wanakuwa na divisheni 1.
Katika mahafali hayo ya mwaka 2025 wanafunzi 56 wamehitimu masomo yao ya kidato cha sita na kukabidhiwa vyeti.
Ends..
0 Comments