WAKUU WA MAJESHI YA NCHI ZA SADC KUKUTANA ARUSHA KESHO,RC MAKONDA ATAKA WANANCHI WASIOGOPE MAGWANDA NA MAGARI YA JESHI,WATUMIE FURSA HIYO KUFANYA BIASHARA

 Na Joseph Ngilisho ARUSHA 


WAKUU wa Majeshi ya Ulinzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajiwa  kukutana kesho mei 26-31 mwaka huu jijini Arusha 


Akiongea na waandishi wa habari leo jumapili Mei 25,2025 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paulo Makonda alisema pamoja na mambo mengine kikao hicho kitapokea na kujadili masuala yote yanayohusu Ulinzi na usalama katika kanda hiyo katika kipindi cha Mwaka mmoja.

Alisema jumla ya Wakuu wa Majeshi  16 kutoka nchi wanachama wa SADC wanatarajiwa kushiriki Kikao hicho ambacho Mwenyekiti wake atakuwa ni Generali Jacob John Mkunda ,Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya wananchi wa Tanzania.

Cdf Jacob Mkunda

Mkuu huyo wa Mkoa alisema mwezi August 2024, rais Samia Suluhu Hassan,  alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC (Chairperson of SADC organ).


"Kutokana na uteuzi huo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania JWTZ, alichukua nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Kikao cha Wakuu wa Majeshi na hiyo ndiyo sababu ya kikao hicho kufanyika hapa nchini"

"Pamoja na ajenda zingine, Kikao hicho kitapokea na kujadili masuala yote yahusuyo Ulinzi na usalama katika kanda kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia May 2024 - May 2025"Alisema Makonda

 

 Makonda alisisitiza  kuwa Arusha imeendelea kuwa kinara wa mikutano ya kitaifa na kimataifa, pamoja na kuwa kitovu cha shughuli za utalii zinazochochea uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla akibainisha kuwa mkutano huo ni fursa nyingine muhimu kwa mkoa kuonyesha uwezo wake katika kutoa huduma bora kwa wageni wa kimataifa.


Alisema kuwa mafanikio haya yanatokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kudumisha amani na utulivu nchini, hali inayowavutia watalii na wawekezaji wengi kufika katika mkoa huo Arusha na kusisitiza kuwa mazingira ya utulivu ndiyo msingi wa maendeleo na kuvutia shughuli kubwa kama hizi za kimataifa.



 Aidha, mapendekezo ya Kikao hicho yatawasilishwa katika Mkutano wa mwaka wa Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano wa masuala ya siasa, ulinzi na usalama (ministerial Committee of Organ) ambao nao utafanyika hapa nchini katika tarehe itakayotangazwa baadaye.



Makonda aliwaomba wananchi wa jiji la Arusha  kuupokea Ugeni huo na kuupa ushirikiano katika kuimarisha ulinzi, na kuutunia kikao hicho  kama fursa ya kutangaza vivutio vya Kiutalii katika Mkoa wetu na Nchi yetu kwa ujumla. 

"Ni imani yangu kuwa tutaichangamkia fursa hiyo ya kuwepo kwa Ugeni huo mzito hapa Mkoani kwetu kwa kufanya biashara mbalimbali"

"Nimalizie kwa kuwashukuru na kuwaomba kuendelea kuziunga mkono Juhudi za Mahususi zinazofanywa na Mhe. Rais Samia za kutuletea fursa kama hizi hapa Mkoani kwetu Arusha"Alisema

Ends....


Post a Comment

0 Comments