NA JOSEPH NGILISHO ARUSHA
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya kimesema kinaridhishwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha inayosimamiwa na mkurugenzi wa jiji hilo Mhandisi Juma Hamsin
Aidha kimesema kinampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika kutafuta fedha Kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kwamba wataendelea kumuunga mkono.
Katibu wa CCM wilaya ya Arusha Timoth Sanga alisema hayo jana wakati wa ziara ya Kamati tendaji ya CCM wilaya ya Arusha iliyotembelea miradi ya Elimu katika shule ya Sekondari Korona,shule ya Sekondari Mrisho Gambo pamoja na kituo cha afya cha Mkonoo.
"CCM wilaya ya Arusha tumeridhishwa na kazi kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo ni miradi ya maendeleo inayotoa huduma kwa wananchi kama ambavyo tuliingia mkataba na wananchi mwaka 2020 wakati wa kuomba ridhaa ya kushika Dola"".
Kuhusu Rais Dk, Samia,Sanga alisema wanampongeza kwa jinsi ambavyo ameonyesha juhudi za dhati katika kuwaletea watanzania maendeleo ya kweli yenye kasi kubwa katika kipindi kifupi cha uongozi wake na kwamba wataendelea kumuunga mkono kwa kuwaeleza wananchi wa wilaya ya Arusha jinsi ambavyo Ilani ya CCM inatekelezwa.
Katika hatua nyingine Sanga alisema wataendelea kuisimamia serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa ili wananchi wapate huduma bora.
"Tumefurahi mno kuona kituo cha afya cha kisasa cha Mkonoo ambacho kinatoa huduma zote muhimu zikiwemo za mama na mtoto bure.Niombe wananchi hasa wanawake wajawazito kuja kutumia huduma za kujifungua pamoja na kuleta watoto wao Kliniki Ili waweze kupata huduma bora ikiwemo elimu ya lishe ambayo ni muhimu sana kwa afya ya mama na mtoto.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Arusha Eliamani Nasari alitoa Rai Kwa wazazi na walezi kuzingatia malezi na makuzi ya watoto Ili wasijiingize kwenye makundi ambayo yanaweza kusababisha wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo yao.
"Tumejiona jinsi ambavyo serikali Kuu imeleta fedha za ujenzi wabweni ya kisasa katika shule ya Sekondari Korona na Mrisho Gambo ambazo ziko pembezoni lengo ni kuhakikisha watoto wanapata elimu.Niwaombe walezi na wazazi wenzangu tuunge mkono juhidi hizi kwa kuhakikisha tunafuatilia Kwa karibu mienendo ya watoto wetu Ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao".
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Ibrahimu Mollel alisema katika shule ya Mrisho Gambo ambapo kunajengwa bweni kupitia fedha za TASAF Halmashauri ya Jiji la Arusha imetoa kiasi cha shilingi milioni Mia Moja na Sitini Kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Bweni hilo pamoja na bwalo la wanafunzi la kulia chakula.
"Halmashauri ya Jiji la Arusha tutaendelea kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo katika Halmashauri yetu.Ili fedha za mapato ya ndani zisaidie kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo katika shule ya Sekondari Korona ambayo ni ya Bweni Halmashauri imeweka taa za kutumia umeme wa jua pamoja na ujenzi wa Bweni moja ambalo ujenzi wake unaendelea".
Awali mkuu wa shule Sekondari Korona Chirstopher Malamsha alisema Mei tano mwaka huu walipokea kiasi cha shilingi milioni 823.6 Kwa ajili ya ujenzi wa mabweni matatu na madarasa mawili pamoja na samani zake ambapo mradi ulikamilika mwezi Agosti na wanafunzi kuanza kutumia mabweni na madarasa hayo Agosti 31 mwaka huu.
"Licha ya fedha hizo mwezi Agosti mwaka huu tumepata fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 130,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Bweni lingine la wanafunzi na ujenzi wake unaendelea na hivi karibuni tutafungua Zahanati ndogo kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi matibabu kutokana na shule yetu kuwa pembezoni".
Naye Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Mkonoo Salum Kobonga alisema anamshukuru Rais Dk, Samia kwa kuleta fedha za ujenzi wa jengo la mama na mtoto,jengo la wagonjwa wa nje pamoja na nyumba ya watumishi (Two in One)
Kata ya Terati ipo pembezoni na Wanawake wengi walikuwa wanajifungulia majumbani lakini baada ya ujenzi wa kituo hicho wameanza kuja kwa wingi kupata huduma za Kliniki,chonjo kwa watoto pamoja na huduma za kujifungua".
...Ends...
0 Comments