Ad
Breaking🔥

STECOL YAONGEZA KASI UJENZI BARABARA MIANZINI-NGARAMTONI

STECOL YAONGEZA KASI UJENZI BARABARA MIANZINI-NGARAMTONI

....Yasema imeondoa vikwazo vilivyokwamisha mradi, mitambo mipya kuwasili kuongeza kasi ya kazi

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


KAMPUNI ya ujenzi ya China, STECOL Corporation, imesema imeongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mianzini hadi Ngaramtoni wilayani Arumeru, mkoani Arusha, baada ya kurejea katika utekelezaji wa kazi Novemba mwaka jana, huku ikiahidi kukamilisha kazi zilizobaki haraka iwezekanavyo.

Meneja wa Mradi wa kampuni hiyo, Yuan Rui alisema tangu kurejea kwao wamefanikiwa kutekeleza kazi mbalimbali katika sehemu kadhaa za mradi huo, ikiwamo sehemu ya kwanza kuanzia eneo la Mezzanine hadi kilomita ya tano kuelekea Anthony, pamoja na maeneo ya sehemu ya tatu, nne na tano.

Rui aliyasema hayo mbele ya Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, alipokuwa katika ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya ujenzi jijini Arusha, ikiwamo mradi huo wa barabara ya Mianzini-Ngaramtoni wilayani Arumeru.

Alisema kampuni hiyo imeongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya ujenzi.

"Tangu Novemba mwaka jana tulipoanza tena kazi, tumefanya juhudi kubwa kuhakikisha tunakamilisha kazi zilizobaki. Kasi yetu sasa ni kubwa kuliko ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita," alisema Rui.

Alisema kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika haraka iwezekanavyo.

Alisema ziara ya Waziri Kadogosa imekuwa muhimu kwa kampuni hiyo kwa kuwa imetoa fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili na kupata maelekezo ya namna ya kuzitatua ili kuharakisha utekelezaji wa mradi.

Katika hatua nyingine, Wang alisema mitambo na vifaa vipya vilivyokuwa vikihitajika katika mradi huo vilikuwa njiani kutoka Dodoma na vilitarajiwa kuwasili eneo la kazi Novemba 24, 2026.

Alisema maandalizi ya mitambo hiyo yanatarajiwa kukamilika kabla ya Ijumaa, Novemba 27, mwaka huu, hatua itakayosaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi.

"Tunafanya kazi kwa ushirikiano na Serikali kuhakikisha changamoto zinatatuliwa. Tutaendelea kufanya juhudi kubwa ili kukamilisha mradi huu haraka iwezekanavyo," alisema Rui.

Alitoa shukrani kwa Waziri Kadogosa kwa kutembelea mradi huo na kufuatilia changamoto zinazowakabili, akisema ushirikiano kati ya Serikali na mkandarasi ni muhimu katika kuhakikisha ujenzi unakamilika.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم