TBA YAANZA OPERESHENI KUWATIMUA WADAIWA SUGU, YADAI WAPANGAJI BIL.6
...Wapangaji wenye madeni kuondolewa nyumba za Serikali, TBA yakusanya Sh250 milioni Dodoma ndani ya siku tatu
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeanza operesheni ya kuwaondoa wapangaji wenye madeni sugu katika nyumba zake nchini, huku ukidai zaidi ya Sh6 bilioni za kodi ya pango kutoka kwa wapangaji mbalimbali.Hatua hiyo inafuatia maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, aliyetaka TBA kuhakikisha wapangaji wanaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi wanaondolewa ili kulinda mali za Serikali na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri Kadogosa kukagua mradi wa ujenzi wa majengo ya makazi na biashara eneo la Kaloleni jijini Arusha, Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Said Mndeme, alisema operesheni hiyo tayari imeanza Dodoma na itasambazwa katika mikoa mingine yenye madeni makubwa.
Alisema mikoa inayolengwa ni pamoja na Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, ambako kuna wapangaji wenye madeni makubwa ya kodi ya pango.
Mndeme alisema kwa sasa TBA inadai takribani Sh6 bilioni kutoka kwa wapangaji wa nyumba zake katika mikoa mbalimbali, huku operesheni iliyoanza Dodoma ikiwa imeanza kuzaa matunda.
Alisema ndani ya siku tatu tangu kuanza kwa operesheni hiyo, zaidi ya Sh250 milioni zilikuwa zimekusanywa hadi jana, akieleza kuwa hatua hiyo itaendelea hadi madeni hayo yatakapopungua kwa kiwango kikubwa.
“Tumepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na tayari tumeanza kuyatekeleza. Operesheni hii itaendelea katika mikoa mingine ikiwemo Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ili kuhakikisha wadaiwa sugu wanaondolewa na madeni yanapungua,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mndeme alisema Waziri Kadogosa ameielekeza TBA kufanya mapitio ya mpango wa uendelezaji wa eneo la Kaloleni ili kuongeza fursa za kibiashara na kuhakikisha mradi huo unakuwa na tija kubwa kiuchumi.
Alisema eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 7,094 limepangwa kujengwa majengo manne yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua familia 400, pamoja na fremu za biashara 152.
Alisema waziri ameitaka TBA kuangalia upya namna ya kuendeleza eneo hilo kwa kuingiza mtazamo wa kibiashara ili kuongeza thamani ya uwekezaji na mapato yatakayopatikana.
Aidha, alisema maelekezo mengine ni kushirikisha benki na taasisi za kifedha katika kugharamia miradi hiyo badala ya kutegemea fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu pekee.
“Tunakwenda kuyafanyia kazi maelekezo hayo kwa kuangalia namna ya kushirikiana na sekta binafsi pamoja na taasisi za kifedha ili kuongeza nguvu katika uendelezaji wa eneo hili na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati,” alisema.
Kuhusu gharama za ujenzi, Mndeme alisema jengo moja katika mradi huo linagharimu Sh6.2 bilioni na linatarajiwa kukamilika Mei 2027, huku Serikali ikiwa tayari imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutachangia kuongeza upatikanaji wa makazi na maeneo ya biashara, sambamba na kuongeza thamani ya eneo la Kaloleni jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake waziri Kadogosa ameipa nguvu TBA kutimua wapangaji wote wadaiwa sugu ili kuwapa wapangaji wengine wenye kuweza kulipa ili wakala huyo aweze kukusanya fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kupeleka miradi kama hiyo maeneo mengi zaidi.
Ends


إرسال تعليق