KADOGOSA ATOA SIKU TATU KULIPA WANANCHI FIDIA YA BILIONI 19 ARUSHA,TANROADS YASEMA INALIPA KESHO
...Aagiza malipo yaanze kesho, Novemba 24; TANROADS yaahidi kuwalipa wananchi waliopitiwa na upanuzi wa barabara
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, ametoa maagizo ya kuanza mara moja kulipwa kwa wananchi wanaostahili fidia ya Sh bilioni 19 katika mradi wa upanuzi wa barabara mkoani Arusha, akitaka zoezi hilo likamilike ndani ya siku mbili hadi tatu ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo.
Kadogosa alitoa maagizo hayo Nov 23,2026 wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Mbauda, jijini Arusha, alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi huo, akisema fedha hizo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba hakuna sababu ya kuendelea kuwachelewesha wananchi kupata haki zao.
"Kwa suala la fidia kwa wananchi wetu hapa, Dkt Samia Suluhu Hassan ameleta Sh bilioni 19. Na hizo fedha kuanzia kesho waanze kuwalipa wananchi. Wekeni timu za kutosha ili ndani ya siku mbili au tatu tuwe tumemaliza," alisema Kadogosa.
Agizo hilo lilipata mwitikio kutoka kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Regnald Masawe, aliyeahidi kuwa taasisi hiyo itaanza kuwalipa wananchi walioathiriwa na upanuzi wa barabara kuanzia kesho, Novemba 24, 2026.
Masawe alisema TANROADS itahakikisha zoezi hilo linaanza kama ilivyoelekezwa, hatua inayolenga kuwaondolea wananchi changamoto zinazohusiana na fidia na kuwezesha shughuli za ujenzi kuendelea kwa kasi.
AWABANA WAKANDARASI KUONGEZA KASI
Katika hatua nyingine, Kadogosa aliwataka wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kuongeza kasi ya kazi kwa kuhakikisha vifaa, mitambo na wafanyakazi vinapatikana kwa wakati, akisema Serikali haitakubali kuona mkandarasi anashindwa kuhamasisha rasilimali za kutosha licha ya mradi kuwa katika hatua za utekelezaji.
Alisema katika ziara yake amekuwa akifuatilia kwa karibu hatua ya maandalizi ya wakandarasi (mobilisation), akieleza kuwa upatikanaji wa vifaa na wataalamu ni msingi wa kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Alizitaja kampuni za CCCC na China Railway kuwa miongoni mwa wakandarasi wanaotekeleza kazi katika maeneo ya mradi huo, huku akiwapongeza kwa hatua ya kuimarisha maandalizi ya kazi.
"Jambo moja ninaloliangalia ni kuhakikisha mnamobilize, yaani mnaleta vifaa vya kufanya kazi, lakini pia mnaleta watu wa kutosha. Sitaki kuja hapa na kuambiwa mkandarasi ameanza kazi lakini mpaka sasa hajamobilize hata asilimia 10. Hilo halikubaliki," alisema.
Kadogosa aliitaka TANROADS, kupitia meneja wa mkoa na vitengo vyake vya usimamizi wa miradi, kuhakikisha inasimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya wakandarasi na washauri elekezi ili kuepusha ucheleweshaji usio wa lazima.
ATOA ONYO KUHUSU UBORA WA BARABARA
Kadogosa pia alisisitiza kuwa Serikali haitakubali mradi huo kutekelezwa kwa viwango vya chini, akiwataka wahandisi na washauri elekezi kuhakikisha kila hatua ya ujenzi inafanyiwa vipimo vya kitaalamu kabla ya kuruhusu hatua inayofuata.
Alisema amekagua baadhi ya kazi zinazofanyika, ikiwamo uwekaji wa maji na uimarishaji wa tabaka la chini la barabara (stabilisation), akitaka uhakiki wa ubora ufanyike kabla ya kuendelea na uwekaji wa tabaka nyingine.
Alisema lengo la Serikali si kujenga barabara kwa gharama kubwa pekee, bali kuhakikisha miundombinu hiyo inakuwa imara, inadumu na inatoa thamani halisi ya fedha za umma zilizotumika.
"Tunachotaka tupate ni ubora unaolingana na fedha zinazotumika. Hatuwezi kukubali barabara inajengwa halafu baada ya mwaka mmoja, miwili au mitatu inaanza kuharibika. Wahandisi mnajua kazi zenu, washauri elekezi wafanye kazi zao na TANROADS isimamie ipasavyo," alisema.
Alibainisha kuwa kwa maelezo ya kiufundi aliyoyapata, barabara hiyo ina matarajio ya kudumu kwa miaka 20, huku sehemu za TRC zikielezwa kuwa na muda wa miaka 50, hivyo akataka viwango hivyo viheshimiwe wakati wote wa utekelezaji.
MRADI WAFIKIA ASILIMIA 54
Akizungumzia kasi ya utekelezaji wa mradi huo, Kadogosa alisema hadi wakati wa ziara yake maendeleo yalikuwa yamefikia asilimia 54, huku matarajio yakiwa kufikia asilimia 56.
Alisema licha ya kuridhishwa na mabadiliko aliyoyaona tangu ziara yake iliyopita, wakandarasi wanapaswa kuandaa mikakati ya kuongeza kasi katika maeneo ambayo bado yako nyuma ya ratiba.
Alisema Serikali haitaridhika na taarifa za maendeleo pekee, bali inataka kuona mabadiliko halisi katika maeneo ya kazi kila anaporejea kufanya ukaguzi.
"Nilipokuja nilikuta sehemu nyingi zikiwa katika hali tofauti, lakini leo nimeona mabadiliko makubwa. Nataka nikirudi tena baada ya wiki kadhaa au mwezi mmoja nikute maendeleo zaidi. Kama tunaenda vizuri nitasema, lakini kama kuna watu wanatuletea matatizo tunajua namna ya kushughulika nao," alisema.
ASEMA RAIS SAMIA ANAIPA ARUSHA KIPAUMBELE
Kadogosa alisema Rais Samia Suluhu Hassan anaipa Arusha umuhimu mkubwa kutokana na nafasi yake katika uchumi wa Taifa, utalii na shughuli nyingine za maendeleo, akieleza kuwa uwekezaji unaofanyika katika miundombinu ya mkoa huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuboresha huduma na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Alisema Rais amewapa viongozi dhamana ya kusimamia miradi kwa niaba ya wananchi, hivyo hawana budi kutekeleza wajibu huo kwa uaminifu, weledi na nguvu zote.
Alisema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi huo na kurejea maeneo mbalimbali kukagua maendeleo, akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na watendaji ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Ends







إرسال تعليق