Ad
Breaking🔥

POLISI KENYA YASHINDWA KUMPELEKA MAHAKAMANI MWANAHARAKATI TWAHA MWAIPAYA

POLISI KENYA YASHINDWA KUMWASILISHA MAHAKAMANI MWANAHARAKATI MTANZANIA

..Mahakama ya Milimani yasubiri uamuzi baada ya maafisa wa polisi kushindwa kueleza alipo Twaha Mwaipaya

By Arushadigital-KENYA

Jeshi la Polisi nchini Kenya limeshindwa kumwasilisha mahakamani mwanaharakati wa kisiasa kutoka Tanzania, Twaha Mwaipaya, licha ya amri ya Mahakama ya Milimani iliyowataka maafisa waandamizi wa jeshi hilo kueleza alipo na kuhakikisha anafikishwa mahakamani.

Mwanaharakati wa haki za binadamu na Mkurugenzi wa Shirika la Vocal Africa, Hussein Khalid, amesema shirika hilo lilikuwepo mahakamani wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya (IG), Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Ruai (OCS) walipotakiwa kumwasilisha Mwaipaya.

Hata hivyo, Khalid amesema maafisa hao wa polisi hawakumwasilisha mwanaharakati huyo, wakieleza kuwa suala lake bado linafanyiwa uchunguzi.

Kutokana na hali hiyo, mahakama imeahirisha shauri hilo huku ikisubiri kutoa uamuzi kuhusu hatua za kisheria zitakazofuata baada ya polisi kushindwa kutekeleza amri iliyotolewa.

"Tunasubiri uamuzi wa mahakama kufuatia polisi kushindwa kumleta Twaha Mwaipaya, akiwa hai au amekufa," amesema Khalid.

Mwaipaya anaripotiwa kutekwa nyara Jumapili, Oktoba 25, 2026, katika eneo la Kamulu, Kaunti ya Nairobi, nchini Kenya, majira ya saa 8:00 mchana.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Amnesty International, magari matatu, likiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop, yalizingira teksi aliyokuwa akisafiria Mwaipaya alipokuwa akielekea kuwatembelea rafiki zake, kisha watu waliokuwa kwenye magari hayo wakamchukua kwa nguvu.

Kwa upande wake, Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya (KNCHR) imesema Mwaipaya alikimbilia nchini humo mwaka 2025 kutokana na hofu ya usalama wa maisha yake nchini Tanzania.

Tume hiyo, kwa kushirikiana na mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu, yakiwemo Defenders Coalition na Linda Mwananchi Movement, imeitaka Serikali ya Kenya kufanya uchunguzi huru na wa haraka kubaini alipo mwanaharakati huyo na kuhakikisha usalama wa wakimbizi wa kisiasa pamoja na watu wengine walio katika mazingira hatarishi.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم