MABADILIKO YA TABIANCHI YATIKISA TANZANIA
...Serikali yataja ukame, mafuriko kuhatarisha kilimo, mifugo na maisha ya wananchi
Yasisitiza taarifa za hali ya hewa kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi kwa wakati
Na Joseph Ngilisho | Arusha
Serikali imesema mabadiliko ya tabianchi yameanza kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya Watanzania, huku ikitaja ukame wa muda mrefu, mafuriko na mabadiliko yasiyotabirika ya mvua kuwa miongoni mwa changamoto zinazotishia usalama wa chakula, maji na uchumi wa wananchi.Kutokana na hali hiyo, Serikali imesema imeweka ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika vipaumbele vyake vya maendeleo, ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utabiri wa hali ya hewa na kuhakikisha taarifa zake zinawafikia wananchi kabla ya majanga kutokea.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akifungua mkutano wa tatu wa wataalamu wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), unaofanyika jijini Arusha , Novemba 02,2026.
Profesa Mbarawa alisema mabadiliko ya tabianchi si tishio la siku zijazo kama ilivyokuwa ikidhaniwa, bali athari zake zinaonekana sasa na kuathiri maisha, shughuli za uzalishaji na uchumi wa nchi mbalimbali, hasa zinazoendelea barani Afrika.
Alisema Tanzania inakabiliwa na vipindi virefu vya ukame, mafuriko yanayosababisha uharibifu na mabadiliko yasiyotabirika ya mifumo ya mvua, hali inayohatarisha uzalishaji wa kilimo, rasilimali za maji, miundombinu na maisha ya wananchi.
"Kwa Tanzania, tunashuhudia ukame wa muda mrefu, mafuriko yenye madhara na mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa. Matukio haya yanatishia uzalishaji wa kilimo, rasilimali za maji, miundombinu na maisha ya wananchi wetu," alisema.
Alisema changamoto hiyo haiwezi kuchukuliwa kama suala la mazingira pekee, bali ni tatizo la maendeleo linalohitaji hatua za pamoja na uwekezaji endelevu ili kulinda maisha ya wananchi na uchumi wa taifa.
ONYO KWA TAASISI
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alizitaka taasisi zinazohusika na masuala ya hali ya hewa na mamlaka za Serikali za mitaa kuhakikisha taarifa za utabiri zinawafikia wananchi kwa wakati, akisema tahadhari isiyomfikia mlengwa haiwezi kusaidia kuokoa maisha.
Alisema Serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa hali ya hewa, teknolojia za utabiri na mifumo ya utoaji wa taarifa za mabadiliko ya tabianchi.
Alisisitiza kuwa taarifa hizo zinapaswa kuandaliwa kwa namna rahisi kueleweka na kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi ambao shughuli zao zinategemea kwa kiasi kikubwa mwenendo wa hali ya hewa.
"Onyo lolote ambalo halimfikii mkulima, mfugaji, mvuvi au jamii iliyo katika mazingira hatarishi haliwezi kuokoa maisha," alisema.
Pia alizitaka taasisi zote husika na wananchi kujiandaa mapema kuelekea msimu wa mvua wa mwaka 2026/2027 kwa kuchukua tahadhari zinazofaa ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu endelevu, nishati jadidifu, teknolojia safi, nishati safi ya kupikia na usafiri wa reli unaotumia umeme.
Alisema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha uchumi huku ukipunguza athari zinazotokana na shughuli za kibinadamu katika mazingira.
Kuhusu mkutano huo wa kimataifa, Profesa Mbarawa alisema majadiliano ya wataalamu wa IPCC na maandalizi ya ripoti ya saba ya tathmini ya mabadiliko ya tabianchi yana umuhimu mkubwa katika kuziwezesha Serikali duniani kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kisayansi.
Alisema matokeo ya tafiti hizo hayapaswi kubaki katika machapisho ya kitaalamu, bali yanapaswa kutafsiriwa katika sera, mipango na uwekezaji unaogusa maisha ya wananchi.
"Sayansi inapaswa kuboresha sera, sera ziongoze uwekezaji na uwekezaji huo hatimaye uboreshe maisha ya wananchi wetu. Hilo ndilo lengo kuu," alisema.
Alisema Tanzania inathamini ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba kuandaa mkutano huo Arusha ni sehemu ya dhamira ya nchi kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto hiyo inayozikabili nchi duniani.
Mkutano huo umekutanisha wataalamu wa kimataifa wa sayansi ya mabadiliko ya tabianchi kujadili masuala mbalimbali yatakayochangia maandalizi ya ripoti ya saba ya tathmini ya IPCC
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ladislaus Chang’a, amesema ongezeko la joto duniani linaendelea kuongeza ukubwa na idadi ya matukio ya hali mbaya ya hewa, hali inayotishia maisha ya wananchi na shughuli za kiuchumi, hususan katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.Chang’a, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi duniani (IPCC), amesema tathmini ya sita ya jopo hilo ilibainisha kuwa joto la dunia limeongezeka kwa takribani nyuzi joto 1.1 za Sentigredi ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Amesema ongezeko hilo la joto linachochea kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa duniani, ikiwemo vipindi vya joto kali na athari nyingine zinazohitaji hatua za haraka za kukabiliana nazo.
Amesema mkutano huo wa siku tano umewakutanisha wanasayansi wabobezi kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza tathmini ya kisayansi kuhusu mwenendo wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani na kutoa mwelekeo wa matukio yanayoweza kujitokeza katika miaka 50 hadi 100 ijayo.
Amesema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo jijini Arusha, ambao ni sehemu ya maandalizi ya tathmini ya saba ya IPCC itakayotoa mwongozo kwa majadiliano na maamuzi ya kimataifa, kikanda na kitaifa kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
"Kadri joto la dunia linavyoendelea kuongezeka, ndivyo changamoto ya matukio ya hali mbaya ya hewa inavyoendelea kuongezeka kwa idadi na ukubwa wake. Afrika pia tunaendelea kukumbana na changamoto hizo," amesema Chang’a.
Amesema ripoti ya kwanza katika tathmini ya saba inatarajiwa kutolewa Machi mwakani, ikiwa itajikita katika namna miji duniani inavyoathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kupunguza athari hizo.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali kuzingatia taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli zao, hususan kilimo, uvuvi na ufugaji, ili kuongeza tija na kupunguza hasara zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Ends



إرسال تعليق