Ad
Breaking🔥

UWANJA WA NDEGE ARUSHA KUFANYAKAZI SAA 24,WAZIRI MBARAWA AZINDUA MIRUKO YA USIKU WAFANYABIASHARA DAVIS MOSHA NA NATHAN KIMARO WAPANDA NDEGE USIKU

ARUSHA SASA KAZI SAA 24, SERIKALI YAWEKEZA SH11 BILIONI

....Mbarawa atangaza viwanja vingine vitano kuanza huduma za usiku, ataka TAA kuvutia mashirika kuongeza safari na mapato

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


SERIKALI imefungua ukurasa mpya wa usafiri wa anga nchini baada ya kuanza rasmi kwa huduma za kutua na kuruka ndege saa 24 katika Uwanja wa Ndege wa Arusha, kufuatia uwekezaji wa takribani Sh11 bilioni katika ufungaji wa mfumo wa taa za kisasa.

Hatua hiyo imehitimisha utaratibu wa uendeshaji wa uwanja huo kwa saa 12 pekee, na sasa ndege zinaweza kutumia miundombinu hiyo usiku na mchana, hatua inayotarajiwa kuongeza shughuli za biashara, utalii na uwekezaji katika Kanda ya Kaskazini.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2023/24 ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea muda wote.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hizo Nov 02,2026, alisema kukamilika kwa mradi huo ni hatua muhimu kwa Arusha, ambayo ni kitovu cha utalii na biashara, huku akieleza kuwa uwekezaji huo unapaswa kuendana na ongezeko la safari na mapato ya uwanja.

“Leo ni siku ya historia. Kwa muda mrefu kiwanja chetu cha ndege cha hapa Arusha kilikuwa kinafanya kazi wakati wa mchana, lakini sasa tunaanza safari za usiku. Maana yake ni kwamba uwanja huu utafanya kazi saa 24 kwa siku, siku saba za wiki,” alisema.

Hata hivyo, Mbarawa alisema kukamilika kwa miundombinu pekee hakutoshi kuhakikisha uwanja unatumika kikamilifu, akilitaka Shirika la Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuweka mikakati ya kuvutia mashirika ya ndege kuongeza safari za usiku.

Alisema TAA inapaswa kufanya mazungumzo na mashirika hayo, kupanga ratiba zinazokidhi mahitaji ya abiria na kuweka mazingira yatakayowashawishi kutumia fursa ya huduma za saa 24.

“Hatuna haja ya kuyasukuma kwa nguvu mashirika ya ndege, bali tunapaswa kuzungumza nayo, kuwa wabunifu na kuweka mazingira yatakayoyafanya yakubali kuendesha safari usiku na mchana,” alisema.

Alisisitiza kuwa uwekezaji wa Sh11 bilioni unapaswa kuleta matokeo yanayoonekana kiuchumi, ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya safari, abiria na mapato ya uwanja huo.

Pia alilitaka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na mashirika mengine kutumia fursa hiyo kuongeza safari, huku akiwahimiza wafanyabiashara wa Arusha kupanua huduma zao hadi nyakati za usiku ili kunufaika na ongezeko la shughuli za usafiri.

Katika kuhakikisha huduma hizo zinaendeshwa kwa usalama, alilitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuimarisha usimamizi wa viwango vya usalama na ubora, akisisitiza kuwa usalama wa abiria na mali zao haupaswi kuathiriwa na kuongezeka kwa muda wa uendeshaji.

VIWANJA VINGINE VITANO KUFUATA

Katika kupanua huduma za usafiri wa anga nyakati za usiku nchini, Mbarawa alisema Serikali ina mpango wa kuongeza viwanja vingine vitano katika mfumo huo.

Alisema viwanja vikubwa vya Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro, Mbeya na Dodoma tayari vina miundombinu ya taa, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha viwanja vingi zaidi vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma hizo.

Alisema lengo ni kuwezesha usafiri wa anga kuchangia uchumi wa saa 24 kwa kurahisisha safari kati ya maeneo mbalimbali nchini na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.

Kuhusu uwezekano wa kupanua Uwanja wa Ndege wa Arusha, alisema Serikali itaendelea kufuatilia ongezeko la idadi ya ndege na abiria kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji mwingine, ili upanuzi wowote uendane na mahitaji halisi.

TAA YAONGEZA WATUMISHI

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo, alisema uzinduzi huo unaashiria kuanza rasmi kwa matumizi ya uwanja huo kwa saa 24, tofauti na awali ambapo huduma zilitolewa kwa muda wa saa 12 pekee.

Alisema TAA imejipanga kuongeza watumishi na kuimarisha mifumo ya kiutendaji ili kuhakikisha huduma za usiku zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya usalama.

“Kwa upande wa uendeshaji tumejipanga kuongeza watumishi ili kuhakikisha shughuli zinaendelea kwa usalama. Pia tumekutana na wadau wa sekta ya usafiri wa anga na kujadiliana namna bora ya kuendesha shughuli hizo kwa saa 24,” alisema.

Mombokaleo alisema Uwanja wa Ndege wa Arusha una uwezo wa kuhudumia ndege za ukubwa wa kati, zikiwamo ATR 72, Q400 na Bombardier.

Alisema TAA inaendelea kushirikiana na mashirika ya ndege kupanga ratiba za safari zitakazowezesha matumizi bora ya miundombinu iliyopo bila kuathiri usalama.

Aliongeza kuwa Uwanja wa Ndege wa Iringa nao umefanyiwa maandalizi ya kuanza kutoa huduma za usiku, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kupanua huduma hizo katika viwanja vya ndege nchini.

WAFANYABIASHARA: SASA MUDA SI TATIZO

Wafanyabiashara wa Arusha wamesema kuanza kwa safari za usiku kutabadilisha namna wanavyotekeleza shughuli zao, hasa safari za kikazi na kibiashara kati ya Arusha na Dar es Salaam, ambazo kwa muda mrefu zililazimika kuzingatia ratiba za mchana.

Mfanyabiashara Nathan Kimaro, anayejishughulisha na biashara ya vifaa vya ujenzi na bidhaa za matumizi ya kila siku (FMCG), alisema huduma hiyo ni hitaji ambalo wakazi wa Arusha wamekuwa wakilililia kwa muda mrefu kutokana na umuhimu wa muda katika biashara.

“Leo ni siku ya kihistoria katika maisha yangu. Nimepata fursa ya kushiriki safari hii ya kwanza ya ndege kuondoka usiku Arusha. Kwa muda mrefu sisi wakazi wa Arusha tumekuwa tukililia fursa hii, lakini sasa tumeipata,” alisema.

Alisema upatikanaji wa huduma hiyo unatoa nafasi kwa wafanyabiashara kutekeleza majukumu yao katika mikoa mbalimbali kwa ufanisi zaidi bila kulazimika kupoteza muda kwa kusubiri safari za siku inayofuata.

Kimaro aliwataka wananchi na wafanyabiashara kutumia fursa hiyo badala ya kusubiri Serikali kufanya kila kitu, akitumia mfano wa mvua inayonyesha na mtu mwenye kiu kushindwa kuchota maji.

“Ukiona mvua inanyesha halafu unalalamika una kiu, hayo ni matatizo yako mwenyewe. Sasa mvua Arusha inanyesha, ni wakati wa kukinga maji na kutumia fursa zilizoletwa,” alisema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara Davis Mosha alisema kuanza kwa safari za usiku kutarahisisha shughuli za kibiashara kwa kuwa wafanyabiashara wataweza kusafiri kutekeleza majukumu yao na kurejea bila kulazimika kusubiri hadi siku inayofuata.

Alisema biashara inahitaji matumizi mazuri ya muda na uhakika wa usafiri, hivyo upatikanaji wa safari za anga saa 24 utaongeza unyumbufu katika kupanga na kutekeleza shughuli za kiuchumi.

“Unaweza kuwa Arusha lakini ukahitaji kufanya biashara Dar es Salaam. Muda ni kitu muhimu sana katika biashara. Unapokuwa na uhakika wa usafiri wakati wowote, unapata nafasi ya kupanga na kutekeleza shughuli zako kwa ufanisi zaidi,” alisema.

Alisema huduma hiyo pia itachochea kuimarika kwa biashara kati ya Arusha na mikoa mingine, huku ikitoa nafasi kwa wafanyabiashara kupanua shughuli zao.

Kwa ujumla, kuanza kwa huduma za usiku katika Uwanja wa Ndege wa Arusha kunafungua fursa mpya kwa sekta ya utalii, hoteli, migahawa, usafiri wa ardhini na biashara nyingine zinazotegemea wageni na wasafiri.

Hata hivyo, utekelezaji wa matarajio hayo utategemea uwezo wa TAA kuvutia mashirika ya ndege, kuongeza safari na kuhakikisha miundombinu iliyowekezwa inatumika kikamilifu.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم