Ad

TAMASHA KUBWA LA SIFA GOSPEL FEST KUTUA KWA KISHINDO ARUSHA,WAIMBAJI MAARUFU WA NYIMBO ZA INJILI KUFUNIKA SINONI

TAMASHA KUBWA LA SIFA GOSPEL FEST KUTUA KWA KISHINDO ARUSHA KUPITIA INJILI NA UIMBAJI

• Vijana kupewa elimu ya ujasiriamali, afya ya akili na ujuzi wa kidijitali

• Rose Mhando, Pendo Nkone, Christine Shushu kuongoza jukwaa

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

WAKAZI wa Jiji la Arusha na viunga vyake wameombwa kujitokeza kwa wingi katika tamasha la Sifa Gospel Fest litakalofanyika Jumamosi Oktoba 10, 2026 katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Sinooni, huku waandaaji wakisema wamekuja na ujumbe wa amani, matumaini, uponyaji na wokovu kupitia muziki wa injili.

Tamasha hilo litakalofanyika kuanzia saa sita mchana hadi saa nne usiku, ni sehemu ya mfululizo wa Sifa Gospel Fest unaofanyika katika mikoa sita nchini, huku Arusha ikiwa ni mkoa wa nne baada ya Mbeya, Geita na Mwanza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sifa Gospel Fest, Suma Mwaitenda, alisema tofauti na mtazamo wa kuona tamasha la muziki wa injili kama burudani pekee, wao wamelenga kulitumia jukwaa hilo kufikisha ujumbe wa kiroho na kijamii kwa makundi mbalimbali, hususan vijana.

Alisema kwa muda mrefu muziki wa injili umekuwa ukikosa majukwaa makubwa yanayoweza kuupa hadhi na nafasi ya kuwafikia watu wengi, jambo lililowasukuma kuanzisha Sifa Gospel Fest.

“Tumekuwa tukiona matamasha makubwa ya nyimbo za kidunia, lakini kwa muda mrefu muziki wa injili umekosa jukwaa kubwa linaloupa thamani. Tunaamini Mungu ametupa neema ya kutengeneza jukwaa hili,” alisema Mwaitenda.

Alisema katika mikoa ambayo wamepita, wamefanikiwa kuwapa nafasi waimbaji na watumishi wapya ambao hawajawahi kupata majukwaa makubwa, hivyo Sifa Gospel Fest imekuwa pia sehemu ya kuibua vipaji vya muziki wa injili.

WAIMBAJI MAARUFU KUPAMBA JUKWAA

Mwaitenda alisema tamasha la Arusha litawakutanisha waimbaji mbalimbali maarufu wa muziki wa injili, akiwamo Pendo Nkone, Christine Shushu, Rose Mhando, Boas Danken, Agape Gospel Band na Neema Gospel Choir, pamoja na waimbaji wengine kutoka Arusha na Mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema ushiriki wa waimbaji hao unalenga kulifanya jukwaa hilo kuwa sehemu ya kuunganisha waimbaji wenye uzoefu na vipaji vipya, huku wananchi wakipata nafasi ya kusikiliza ujumbe wa injili kupitia muziki.

VIJANA WAWEKWA MBELE

Mwaitenda alisema baada ya kubaini kuwa vijana ndiyo kundi kubwa linalojitokeza katika matamasha hayo, waandaaji wameamua kuunganisha huduma ya injili na elimu ya maisha.

Alisema Ijumaa Oktoba 9, siku moja kabla ya tamasha kuu, watafanya programu maalumu kwa vijana katika Plush Gardens, Arusha, itakayojikita katika ujasiriamali, afya ya akili, ujuzi wa kidijitali na namna ya kurasimisha biashara.

Kwa mujibu wake, wadau mbalimbali wakiwamo Equity Bank na BRELA wamealikwa kushiriki kutoa elimu kwa vijana wanaofanya biashara, wahitimu wa vyuo na wale ambao bado hawajapata ajira.

“Tumewaona vijana wana matatizo kwenye biashara zao lakini wanashindwa kupata mahali pa kupata majibu. Tukaona tulete neema ya injili, lakini pia tutoe nafasi kwa vijana kupata maarifa ya kutengeneza leo yao na kesho yao,” alisema.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma inayotolewa na Sifa Gospel Fest haigusi eneo la kiroho pekee, bali pia inagusa changamoto za kijamii na kiuchumi zinazowakabili vijana.

‘HAKUNA KIINGILIO’

Akijibu hoja kuhusu tofauti kati ya Sifa Gospel Fest na baadhi ya mikusanyiko ya kidini inayotuhumiwa kugeuzwa kuwa sehemu za biashara, Mwaitenda alisema tamasha hilo halina kiingilio wala halilengi kufanya biashara kwa kutumia waumini.

“Hakuna kiingilio, hatuuzi chochote zaidi ya Neno la Mungu ambalo ni bure kwa waamini na wasio waamini. Ni ibada ya kusifu na kuabudu,” alisema.

Alisema tamasha hilo linaendeshwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, akiwataja Timeless Expedition, Talanta Sports and Events, Event Set, Clouds Media Group na Global TV.

Alisema wafanyabiashara wanaweza kutumia fursa ya uwepo wa watu wengi kuuza bidhaa halali kama maji, juisi na vyakula, lakini biashara si lengo la msingi la tamasha hilo.

UJUMBE WA AMANI, MATUMAINI



Mwaitenda alisema uzoefu walioupata katika mikoa ya Mbeya, Geita na Mwanza umeonyesha kuwa muziki wa injili unaweza kuwa njia yenye nguvu ya kuwafikia vijana ambao wakati mwingine ni vigumu kuwafikia kupitia njia nyingine za kawaida za uinjilisti.

Alisema ujumbe wanaolenga kuufikisha kupitia Sifa Gospel Fest ni wa amani, matumaini, wokovu na uponyaji.

“Tunaamini katika uimbaji watu wanafunguliwa, watu wanaamini tena, watu wanapona na kama walikuwa na majeraha wanakuwa watu wapya,” alisema.

Alisema jukwaa hilo pia linatoa nafasi kwa waimbaji wapya kuonyesha vipaji vyao na kufikisha ujumbe kwa maelfu ya watu wanaohudhuria moja kwa moja na wengine wanaofuatilia kupitia vyombo vya habari.

Mwaitenda aliwataka wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani, wakiwamo vijana, wazazi, watoto, waamini na wasio waamini, kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo.

“Tunawaalika wana Arusha wote. Njoo usikilize ujumbe, furahia vipaji na upate nafasi ya kushiriki katika huduma hii,” alisema.

Ends 

Post a Comment

أحدث أقدم