TAHA YABADILI KILIMO ARUMERU, WAKULIMA 1,200 WANUFAIKA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MKURUGENZI Mtendaji wa Tanzania Horticultural Association (TAHA), Dkt. Jacqueline Mkindi, amesema uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji umeanza kubadili maisha ya wakulima katika Jimbo la Arumeru Magharibi, ambako zaidi ya wananchi 1,200 wananufaika na mradi wa mfereji unaofadhiliwa na taasisi hiyo.
Dkt. Mkindi alisema hayo OKTOBA 6,2026 baada ya wajumbe wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kutembelea mradi huo na kujionea namna unavyowawezesha wananchi kufanya kilimo cha umwagiliaji, ikiwemo uzalishaji wa vitunguu na mazao mengine ya bustani.
Alisema upatikanaji wa maji ya uhakika umewawezesha wakulima kuongeza maeneo ya uzalishaji, kulima kwa misimu inayofuatana na kuongeza kipato, huku vijana wakipata fursa za ajira katika shughuli za kilimo.
“Jukumu letu ni kusaidia maendeleo na mabadiliko ya sekta ya kilimo cha bustani. Tunafanya kazi kwa karibu sana na Serikali kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa rafiki kwa wakulima na sekta binafsi,” alisema Dkt. Mkindi.
Alisema TAHA pia inaendelea kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa uzalishaji wenye tija lazima uendane na upatikanaji wa masoko.
“Katika kilimo huwezi kuzungumzia mnyororo wa thamani wenye ushindani bila masoko na biashara. Sisi tunafungua masoko, tunawezesha biashara na tunabaini fursa za uwekezaji,” alisema.
Alisema taasisi hiyo imekuwa ikifanya tafiti za masoko na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya kimataifa, ikiwemo India, huku ikilenga kuongeza uzalishaji na ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la dunia.
Kwa upande wake, mkulima Godlizen Michael Mollel, mnufaika wa mradi huo, alisema mfereji huo umeondoa changamoto ya ukosefu wa maji na kuwawezesha kutumia eneo kubwa zaidi kwa kilimo.“Kwa kweli mradi huu tumenufaika sana. Awali tulikuwa na eneo kubwa la kulima, lakini tulikuwa tunakosa maji ya uhakika. Sasa tunapata maji ya kumwagilia, matumizi ya nyumbani na hata kwa ajili ya mifugo,” alisema Mollel.
Alisema wakulima sasa wanaweza kulima mazao tofauti kwa misimu inayofuatana, ikiwemo mahindi na kabichi, hali inayoongeza uzalishaji na kipato cha kaya.
Wakati huohuo, wajumbe wa IPU waliipongeza TAHA kwa kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wakisema ziara yao imewapa matumaini baada ya kujionea namna Serikali, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi zinavyoshirikiana kuboresha maisha ya wananchi.
Mwakilishi wa IPU alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo yanayoonekana kwa jamii.







إرسال تعليق