DC LUGANGIRA: TUJIANDAE NA ARUMERU YA KIMATAIFA
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MKUU mpya wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ameahidi kuleta kasi mpya katika utendaji wa Serikali wilayani humo, akitaja kuimarisha usalama, kutatua kero za wananchi, kusimamia miradi ya maendeleo na kukuza uchumi kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake.
Lugangira ametoa kauli hiyo OKTOBA 3,2026 muda mfupi baada ya kuapishwa kushika nafasi hiyo, akisema amepokea dhamana aliyopewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa unyenyekevu mkubwa na yuko tayari kushirikiana na wananchi na viongozi wote kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa.
Amesema kabla ya uteuzi huo alikuwa akitekeleza majukumu nje ya nchi, lakini baada ya kupata wito wa kulitumikia Taifa kupitia uteuzi wa Rais, alisitisha mkataba wake na kurejea Arusha kwa ajili ya kuanza majukumu mapya.
“Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi ambao amenipatia wa kumsaidia kwenye wilaya yetu ya Arumeru,” amesema Lugangira.
Amesema dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wa Arumeru wanapata viongozi wanaowasikiliza, wanaowafikia na wanaochukua hatua katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Kwa mujibu wa Lugangira, usalama wa wananchi utakuwa miongoni mwa maeneo yatakayopewa uzito katika uongozi wake, sambamba na kuhakikisha wananchi wanatambua kuwa viongozi wapo kwa ajili yao.
“Tunakwenda kuimarisha usalama kwenye wilaya yetu ya Arumeru, lakini pia tunakwenda kuhakikisha wananchi wanajisikia kwamba viongozi tupo kwa ajili yao kutatua kero zote za wananchi wetu,” amesema.
Katika eneo la maendeleo, Rugangira amesema atahakikisha miradi inayotekelezwa wilayani humo inasimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatimiza malengo yaliyokusudiwa na wananchi wanapata thamani ya uwekezaji huo.
Pamoja na hayo, amesema ataweka mkazo katika kuimarisha uchumi wa Arumeru, hasa kupitia ongezeko la mapato ya wilaya, akieleza kuwa uchumi imara ni sehemu muhimu ya kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akiwahutubia wananchi wa Arumeru, Lugangira amewataka wamchukulie kama mtumishi wao na si kiongozi aliye mbali nao, huku akiwaomba wasisite kumuelekeza pale wanapoona kuna jambo linalohitaji kurekebishwa.
“Mimi kama Mkuu wa Wilaya ya Arumeru naomba niwaambie wana Arumeru wenzangu kwamba wao ndio viongozi wangu. Mimi nimekuja kwa ajili ya kuwatumikia wana Arumeru,” amesema.
Ameongeza:
“Naomba ushirikiano, nawaomba msisite kunielekeza, nawaomba tutembee pamoja, maana pale ambapo tutatembea pamoja ndipo tutaweza kutimiza malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na kuifikisha wilaya yetu pale ambapo ndiyo matarajio ya kiongozi wetu mkuu wa Taifa.”
Katika kauli yake iliyobeba taswira ya matarajio yake kwa wilaya hiyo, Rugangira amesema anataka wananchi na wadau mbalimbali waanze kujiandaa kwa Arumeru yenye nafasi kubwa zaidi katika maendeleo.
“Kwanza kabisa, tujiandae na Arumeru ya kimataifa,” amesema.
Aidha, akisisitiza umuhimu wa viongozi kufuatilia utekelezaji wa mipango na miradi kwa vitendo badala ya kutegemea taarifa za ofisini pekee, Rugangira amesema:
“Jambo la pili na la muhimu, naomba niseme, tukutane site.”
Kauli hiyo imeashiria msisitizo wake wa kwenda katika maeneo ya utekelezaji wa miradi na kukutana moja kwa moja na wananchi ili kufahamu changamoto zao na kufuatilia hatua zinazochukuliwa na Serikali.
Lugangira amesema mafanikio ya Arumeru hayawezi kujengwa na mtu mmoja, bali yanahitaji ushirikiano wa wananchi, viongozi wa Serikali, watendaji, taasisi na wadau wengine, akisisitiza kuwa mshikamano huo ndiyo njia ya kufikia malengo yaliyowekwa.
Ends

Post a Comment