Ad
Breaking🔥

RC AWATAHADHALISHA WATEULE YEYE NI MWAKILISHI WA RAIS LAZIMA WATII MAELEKEZO YAKE.,AAPISHA MA -DC WAPYA ARUSHA, ATAKA WASIJIONE WAKUBWA WATUMIKIE WANANCHI ...'MNADENI KUBWA'

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Amos Makala, amewataka Wakuu wapya wa Wilaya kutambua kuwa uteuzi wao si tuzo ya kujivunia wasifu binafsi, bali ni dhamana kubwa ya kuwatumikia wananchi waliyopewa kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.

Makala alisema viongozi hao wanapaswa kuanza safari yao ya uongozi kwa kumshukuru Mungu na kutambua uzito wa nafasi walizokabidhiwa, akisema kati ya Watanzania zaidi ya milioni 60, wao wameaminiwa kushika dhamana hiyo.

“Watanzania ni zaidi ya milioni 60. Kwa nini wewe? Ukiongozwa na hilo, ongea na Mwenyezi Mungu. Mwisho wa yote una deni la kutumikia wananchi. Mungu amepanga wewe uwe mtumishi wa wananchi,” alisema Makala.

Kauli hiyo aliitoa OKTOBA 3,2026 wakati wa hafla ya uapisho wa Wakuu wapya watatu ,Nicodemus Mwikozi DC Arusha,Neema Rugangila DC Arumeru na Luten Robert  Kakomagile ,DC Ngorongoro katika Mkoa wa Arusha, ambapo aliwataka viongozi hao kutotafsiri uteuzi wao kama matokeo ya uwezo wao binafsi, wasifu au nafasi walizowahi kushika, bali kama dhamana ya Serikali inayopaswa kuthibitishwa kwa matokeo.

“Napenda kuwapongeza, lakini si kwa uwezo wenu wala CV zenu. Mungu kupitia Dkt Samia Suluhu Hassan ndiye aliyewateua kuwa Wakuu wa Wilaya. Kwa hiyo pokeeni nafasi hizi mkijua kuna majukumu makubwa mmepewa,” alisema.

Makala alisema Serikali ya Mkoa ipo tayari kushirikiana na viongozi hao, akiwataka kwenda kwa wananchi, kusikiliza changamoto zao na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mipango na miradi ya Serikali.

“Mimi ndiye kiongozi wenu wa shughuli zote za Serikali katika mkoa wangu. Msaidieni kazi. Mimi nawaahidi ushirikiano mzuri wa kuwalea ili muendelee kuchapa kazi na baadaye muendelee kuwa na nafasi mbalimbali,” alisema.

Makala aliwataka Wakuu hao wa Wilaya kutambua kuwa nafasi walizopewa si mwisho wa safari ya utumishi wa umma, akisisitiza kuwa wanapaswa kutumia uzoefu, nguvu na maarifa yao katika kutatua changamoto za wananchi badala ya kujiona bora kuliko wengine.

Alisema baadhi yao wana uzoefu mkubwa katika utumishi wa umma, huku wengine wakiwa vijana wenye nguvu na uwezo wa kufika vijijini na kufuatilia moja kwa moja changamoto zinazowakabili wananchi.

“Dhamana ya uongozi inapimwa kwa matokeo. Nendeni mkafanye kazi na wananchi, siyo kwenda kujenga majina yenu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Makala alisema Arusha ina nafasi ya kipekee katika uchumi na diplomasia ya Tanzania kutokana na kuwa kitovu cha utalii, mikutano ya kimataifa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema historia ya Arusha katika diplomasia ni kubwa, akitaja miongoni mwa mambo yaliyofanyika mkoani humo ni juhudi za kuleta amani katika migogoro ya Rwanda na Burundi.

“Arusha ni mkoa mkubwa. Ni kitovu cha diplomasia. Hapa ndipo yalipopatikana makubaliano ya amani ya Rwanda na Burundi. Hapa pia ndipo makao makuu ya Afrika Mashariki na ni kitovu cha utalii,” alisema.

Alisema fursa hiyo inapaswa kutumiwa kikamilifu kukuza uchumi wa wananchi kupitia utalii wa kawaida na utalii wa mikutano, akisisitiza kuwa wageni wanaofika Arusha kwa shughuli za kimataifa pia hutumia huduma mbalimbali na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Paulo Makonda, amewataka Wakuu wapya wa Wilaya kuunganisha nguvu na viongozi wengine kuhakikisha Jiji la Arusha linapata maendeleo, usafi, amani na mazingira bora ya biashara na uwekezaji.

Makonda alisema Arusha imekuwa nyuma kwa muda mrefu katika baadhi ya maeneo ya miundombinu, hivyo ujio wa viongozi wapya unapaswa kwenda sambamba na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza na Mkuu mpya wa Wilaya ya Arusha Mjini, Makonda alisema anatarajia kiongozi huyo kushirikiana kwa karibu na Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wengine kuhakikisha mipango ya Serikali na mahitaji ya wananchi yanatekelezwa kwa kasi.

“Tunataka kuona maendeleo. Tumebaki nyuma muda mrefu sana. Tumekuwa na changamoto za barabara, hatuna stendi, hatuna soko na hata jengo la utawala la jiji letu lilikuwa changamoto. Kwa hiyo kuwepo kwako hapa tunayo imani kwamba utamsaidia Mkuu wa Mkoa kutimiza maono ya Dkt Samia na wananchi wa Arusha,” alisema.

Makonda pia alisisitiza suala la usafi wa Jiji la Arusha, akisema hadhi ya mji huo kama kitovu cha mikutano ya kimataifa inahitaji mazingira safi, salama na yenye kuvutia.

“Tunaumia kuona jiji letu kutokuwa safi. Dunia nzima inakuja hapa Arusha, kwa hiyo lazima tutengeneze mazingira yanayofaa,” alisema.

Alisema fursa zinazotokana na mikutano ya kimataifa, michezo na shughuli nyingine zinapaswa kutumiwa kuwawezesha wafanyabiashara, wajasiriamali, waendesha pikipiki na wananchi wengine kunufaika kiuchumi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu, akisema maendeleo hayawezi kupatikana bila mazingira salama kwa wananchi kufanya shughuli zao.

“Tunataka maendeleo, usafi, amani na mshikamano. Tukiviunganisha vitu hivi, tunaweza kuona Arusha yetu inakwenda vizuri,” alisema.

Makonda aliwataka viongozi wapya kujenga utamaduni wa kukutana, kujadiliana changamoto na kutafuta suluhisho kwa pamoja, akiahidi ushirikiano kutoka kwake, madiwani na viongozi wengine wa Jiji la Arusha.

Ends


Post a Comment

Previous Post Next Post