SABAYA: KIFO HAKICHAGUI CHAMA WALA CHEO
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu wanapofariki, badala ya kuwafariji wafiwa na kuheshimu kumbukumbu za marehemu, huanza kujadili vifo vyao kwa misingi ya kisiasa au sababu nyingine zisizothibitishwa.
“Kifo ni mjumbe katili sana. Kikija kwa wakati wake, lazima kifike. Uwe CCM, Chadema, uwe kiongozi au mtu wa kawaida, kifo hakichagui,” alisema Sabaya.
Alisema amekutana na marehemu Sikoi mara moja tu maishani, lakini katika mazungumzo yao alibaini kuwa alikuwa mtu mwenye imani kubwa kwa Mungu na matumaini ya kupona.
Sabaya alisema licha ya marehemu kuwa na imani hiyo, kifo chake ni sehemu ya mapenzi ya Mungu, akiwataka wananchi kujifunza kuthamini maisha na kuonesha upendo kwa wenzao wangali hai.
Katika salamu zake za rambirambi, Sabaya alisema amepata pigo la kupoteza viongozi wawili ndani ya wiki moja, akiwemo mwenyekiti na mjumbe, hali iliyomfanya kutoa wito wa kuwaombea viongozi wengine ili waendelee kuwa salama.
Alisema licha ya kushiriki katika siasa, imani yake kwa Mungu ni sehemu muhimu ya maisha yake, ndiyo maana haoni sababu ya kutenganisha mazungumzo ya kisiasa na ujumbe wa kiroho, hasa wakati wa kuomboleza.
Akitoa salamu za mwisho kwa marehemu Sikoi, Sabaya alisema anaamini kuwa siku moja watakutana tena katika ufalme wa Mungu, ambako hakutakuwa na tofauti za vyama vya siasa, mauti wala uharibifu.
Alitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wa Kata ya Olorien kutokana na msiba huo, huku akiwaomba waendelee kuwa na imani katika kipindi hiki kigumu.Ends













إرسال تعليق