POLISI KANDA YA KASKAZINI KUWANASA MADEREVA WALEVI, WANAOENDESHA KWA KASI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
JESHI la Polisi Kanda ya Kaskazini limeonya madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote wanaohatarisha maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Onyo hilo limetolewa wakati jeshi hilo likiimarisha operesheni za pamoja za ukaguzi na udhibiti wa makosa ya barabarani katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara, baada ya kubaini ukiukwaji wa sheria ikiwemo mwendokasi, ulevi wakati wa kuendesha na kuzidisha abiria.
Akizungumza wakati wa operesheni iliyofanyika usiku wa Oktoba 20, 2026, eneo la Kikatiti, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, SSP Nassoro Sisiwaya, alisema madereva wanaokiuka sheria hizo wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.Alisisitiza kuwa usalama barabarani ni wajibu wa kila dereva na kwamba hakuna sababu inayopaswa kutumiwa kuhalalisha vitendo vinavyohatarisha maisha ya watu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, ACP Zauda Mohamed, aliwataka madereva wa magari ya abiria kuhakikisha wanapata muda wa kutosha wa kupumzika baada ya safari ndefu ili kuepuka ajali zinazoweza kusababishwa na uchovu.
Alisema tahadhari hiyo ni muhimu zaidi katika kipindi hiki cha kufunguliwa kwa vyuo, ambapo idadi ya abiria na safari huongezeka, hivyo kuhitaji madereva kuzingatia nidhamu, umakini na muda wa mapumziko.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, SSP William Mwamasika, alisema operesheni hizo zimebaini makosa mbalimbali, yakiwemo mwendokasi, kubeba abiria kupita kiasi, kupita magari mengine bila tahadhari, kuendesha gari ukiwa umelewa, kutumia magari yenye hitilafu na kutokuwa na vifaa vya kuakisi mwanga nyuma ya magari.
Alisema hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya madereva waliobainika kukiuka sheria, ikiwemo kutozwa faini na kufungiwa leseni pale inapostahili.
Akitoa wito kwa madereva na wamiliki wa magari, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Manyara, SP Michael Mwakasungula, aliwataka kuhakikisha magari yanafanyiwa matengenezo kwa wakati na kuwa katika hali nzuri kabla ya kuruhusiwa barabarani.
Alisisitiza kuwa madereva wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya usalama barabarani, akieleza kuwa uzembe wa dereva mmoja unaweza kuhatarisha maisha ya abiria wengi na watumiaji wengine wa barabara.
Operesheni hizo ni endelevu na zitaendelea katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti makosa ya barabarani, kuimarisha nidhamu ya madereva na kulinda maisha ya wananchi.
Ends

إرسال تعليق