Ad
Breaking🔥

WAFANYAKAZI ARUSHA SUNDRIES WAGOMA, WADAI KUPUNJWA MALIPO YAO WAMTUHUMI MENEJA WAO SULEIMAN KWA KUWATUKANA MATUSI YA NGUONI NA KUWADHALILISHA

 WAFANYAKAZI ARUSHA SUNDRIES WAGOMA, WADAI KUPUNJWA MALIPO

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA



WAFANYAKAZI wa kampuni ya usambazaji wa bidhaa za madukani ya Arusha Sundries, iliyopo eneo la Majengo Juu jijini Arusha, wamegoma kufanya kazi wakidai kulipwa ujira mdogo, kutukanwa na kunyimwa mikataba ya ajira kwa muda mrefu.



Wakizungumza kwa jazba nje ya kituo chao cha kazi,Leo OKTOBA 22,2026 wafanyakazi hao walimtuhumu meneja mauzo wa kampuni hiyo tawi la Arusha, aliyemtaja kwa jina  la Suleiman Said, kudaiwa kutumia lugha chafu na matusi wanapowasilisha malalamiko yao kuhusu mazingira ya kazi.

Mmoja wa wafanyakazi hao, Abillah Juma, alisema wanafanya kazi ngumu ya kupakua bidhaa na kuzipanga ghalani, lakini hulipwa Sh11,000 kwa siku, kiasi ambacho wanadai hakikidhi mahitaji yao ya msingi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Alisema wamekuwa wakitaka malipo yao yaongezwe hadi Sh15,000 kwa siku ili yaendane na ugumu wa kazi wanazofanya na kuwasaidia kumudu mahitaji ya kila siku.

Mfanyakazi mwingine, Hasan Juma, alisema licha ya kulalamikia kiwango cha malipo, pia wanakabiliwa na changamoto ya kukosa mikataba ya ajira, huku baadhi yao wakidai wamefanya kazi katika kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka minne bila kupewa mikataba.

Alidai kuwa malipo yao hutolewa tarehe 15 na 30 ya kila mwezi, huku akimtuhumu meneja huyo kuwatukana kwa lugha za kudhalilisha wanapodai haki zao.

Wafanyakazi hao wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo ili madai yao yasikilizwe, haki zao zilindwe na hatua stahiki zichukuliwe endapo itabainika kuwa kuna ukiukwaji wa sheria za kazi.

                             
SULEIMAN,Meneja mauzo -SUNDRIES 

Akijibu malalamiko hayo, Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Suleiman, alisema madai ya wafanyakazi hao yanaendelea kushughulikiwa, akieleza kuwa suala hilo haliwezi kutatuliwa kwa siku moja kwa kuwa mmiliki wa kampuni yupo nje ya nchi.

Aliahidi kutoa majibu kuhusu madai hayo Jumatatu, huku akikanusha tuhuma za kuwatolea wafanyakazi lugha chafu.

Hata hivyo, Suleiman alikiri kuwa wafanyakazi hao hawajaajiriwa rasmi, akieleza kuwa ni vibarua wanaolipwa kwa siku.

.....Ends.....

Post a Comment

أحدث أقدم