Ad
Breaking🔥

LUKUMAY AIPONGEZA TAHA MRADI WA UMWAGILIAJI WAZALISHA AJIRA, MAVUNO YAONGEZEKA,AITAKA SERIKALI KUJENGA ‘COLD ROOMS’ ILKIDING’A

 Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, amepongeza Chama cha wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA) kwa utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji na kilimo cha mbogamboga katika Kata ya Ilkiding’a, akisema umefungua fursa za ajira na biashara kwa vijana na kuongeza uzalishaji wa mazao.




Dkt Lukumay aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani waliotembelea mradi huo unaotekelezwa kwa ufadhili wa TAHA kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP) na Mastercard.

Alisema mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh213 milioni, kwa sasa unawanufaisha wakulima wapatao 1,200 wanaolima katika eneo lenye takribani ekari 315.




“Napenda kutumia nafasi hii kuishukuru sana TAHA kwa kazi nzuri iliyofanya hapa. Mradi huu umeongeza ajira kwa vijana wetu na kuwawezesha kuingia katika kilimo biashara,” alisema Dkt Lukumay.

Alisema mafanikio ya mradi huo yanaonekana kupitia ongezeko kubwa la uzalishaji wa vitunguu, akibainisha kuwa miaka miwili iliyopita mkulima aliweza kupata wastani wa magunia 15 kwa ekari moja, lakini kwa sasa uzalishaji umefikia zaidi ya magunia 50 kwa ekari.

Dkt Lukumay alisema mafanikio hayo yanaifanya kilimo kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa vijana, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo ili wakulima waweze kunufaika zaidi na uzalishaji wao.

Katika hatua nyingine, Dkt Lukumay alisema ameiomba Serikali kupitia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kujenga vyumba maalumu vya kuhifadhia mazao kwa baridi (cold rooms) ili kuwasaidia wakulima kuhifadhi mazao yao baada ya kuvuna na kupunguza hasara.

Alisema ombi hilo tayari limepokelewa na viongozi wa Serikali, akiwamo Waziri wa Kilimo, ambaye ameonyesha utayari wa kushughulikia suala hilo.

“Nililiomba Serikali hawa wakulima wapatiwe vyumba vya baridi vya kuhifadhia mazao yao, vinavyojulikana kama cold rooms. Nimefurahi kuona kwamba viongozi na Waziri wa Kilimo wamepokea hoja hii na wameahidi kushughulikia ujenzi wa miundombinu hiyo,” alisema.

Dkt Lukumay pia aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika shughuli za uzalishaji, akisema ushirikiano huo unaonekana kupitia utekelezaji wa miradi kama huo wa Ilkiding’a.

Aidha, aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani nchini ili Tanzania iendelee kuwa mazingira salama kwa wawekezaji, wafadhili na mashirika ya kimataifa kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Wito wangu kwa Watanzania ni kuendelea kudumisha amani katika nchi yetu ili miradi kama hii iweze kuendelea. Wafadhili na wadau wetu wa kimataifa, ikiwamo WFP na mashirika mengine, waweze kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dkt Lukumay alimtakia Rais Samia Suluhu Hassan afya njema na kuendelea na juhudi za kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Aliwashukuru pia wananchi wa Kata ya Ilkiding’a kwa kujitokeza kwa wingi kuwapokea viongozi wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali waliotembelea mradi huo, pamoja na wote walioshiriki katika maandalizi ya ziara hiyo.

Ends .

Post a Comment

Previous Post Next Post