DC ARUMERU ATOA MAAGIZO SITA, AONYA WAZEMBE
...Aitaka Arusha DC, Meru DC kupata hati safi za CAG
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ametoa maagizo sita kwa watendaji wa serikali katika Wilaya ya Arumeru, akisisitiza ulinzi na usalama, utatuzi wa kero za wananchi, migogoro ya ardhi, usafi na utunzaji wa mazingira, usimamizi wa miradi ya maendeleo na udhibiti wa fedha za umma.
Lugangira alisema hatavumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma, akitaka viongozi kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora, za haki na zinazopimika kwa matokeo.
Akizungumza na watumishi na viongozi wa wilaya hiyo,baada ya kukabidhiwa ofisi Oktoba 9,2026, alisema amepokea dhamana kubwa kutoka kwa Rais, hivyo anatarajia ushirikiano wa dhati katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Arumeru.
Alisema ukubwa wa majukumu yake ni mkubwa kutokana na eneo la kiutawala analoliongoza, lenye halmashauri mbili za Arusha DC na Meru DC, majimbo mawili ya Arumeru Magharibi na Arumeru Mashariki pamoja na kata nyingi.
“Nimepewa dhamana kubwa na heshima kubwa na Mheshimiwa Rais. Ninaamini tutashirikiana pamoja kwa ajili ya Arumeru yetu,” alisema.
Lugangira, ambaye alisema amefanya kazi katika sekta binafsi, serikalini, Bungeni na taasisi za kimataifa, alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ubunifu na uongozi unaozingatia matokeo yanayoweza kupimwa.
Alisema anahitaji taarifa sahihi kutoka kwa watendaji, badala ya taarifa zinazolenga kumfurahisha, akitaka changamoto zinazoripotiwa ziambatane na mapendekezo ya namna ya kuzitatua.
“Natamani kupata taarifa sahihi, si taarifa za kunifurahisha. Kama kuna changamoto, nataka ziambatane na mapendekezo ya suluhisho,” alisema.
Katika maagizo yake, Lugangira alitaja ulinzi na usalama kuwa kipaumbele cha kwanza, akieleza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na kuwataka viongozi kushirikiana na wananchi kuzuia matukio ya uhalifu.
Alisema matukio ya mauaji na vitendo vingine vinavyotishia usalama yanahitaji ushirikiano wa viongozi, vyombo vya usalama na jamii ili kuhakikisha wananchi wanaishi na kufanya shughuli zao kwa amani.
Agizo la pili lilihusu utatuzi wa kero za wananchi, ambapo alielekeza kuwepo kwa siku moja kila wiki ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko katika ngazi za vijiji na kata.
Alitaka kila kero iwe na kumbukumbu, hatua zilizochukuliwa na mrejesho kwa mhusika, akisisitiza kuwa watendaji wanapaswa kuwajibika katika kuhakikisha malalamiko hayapuuzwi.
Kuhusu migogoro ya ardhi, alisema inapaswa kutatuliwa mapema, kwa haki na kwa kuzingatia sheria ili kuzuia migogoro inayoweza kushughulikiwa kiutawala isigeuke kuwa tishio kwa amani.
Katika eneo la usafi na utunzaji wa mazingira, aliwataka viongozi kuhakikisha vijiji, kata, masoko na maeneo ya biashara yanakuwa safi, huku wakisimamia uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira.
Agizo la tano lilihusu usimamizi wa miradi ya maendeleo, ambapo alisema kila mradi lazima ukamilike kwa ubora unaotakiwa, kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotumika.
Alisema hatakubali miradi ambayo gharama zake hazilingani na kazi iliyofanyika, akiwataka viongozi wa vijiji, kata na tarafa kufuatilia utekelezaji wa miradi katika maeneo yao na kutoa taarifa mapema pale changamoto zinapojitokeza.
Agizo la sita lilihusu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo aliwataka wakurugenzi wa halmashauri hizo mbili kuimarisha nidhamu ya fedha, mifumo ya udhibiti wa ndani na kushughulikia hoja za ukaguzi kwa wakati.
“Lengo langu ni kuhakikisha halmashauri zangu zote mbili, Arusha DC na Meru DC, zinapata hati safi wakati wa ukaguzi,” alisema.
Lugangira pia alisisitiza kupambana na rushwa, kuondoa urasimu usio wa lazima na kukomesha vitendo vya dharau kwa wananchi, akieleza kuwa kila mtu anapaswa kupata huduma kwa usawa bila kujali nafasi yake au watu anaowafahamu.
Alisema watumishi wa umma wanapaswa kuwahudumia wananchi kwa heshima katika ofisi, hospitali na taasisi nyingine za serikali.
“Wananchi ndiyo waliotuweka hapa. Sisi tuko hapa kwa ajili ya kuhakikisha tunawatumikia wao,” alisema.
Ends



Post a Comment